Arusha
Home » » RAIS KIKWETE, LOWASSA KUGAWA NG’OMBE KWA WAFUGAJI

RAIS KIKWETE, LOWASSA KUGAWA NG’OMBE KWA WAFUGAJI



Na Eliya Mbonea, Arusha
FAMILIA zaidi ya 125 wilayani Monduli na Ngorongoro mkoani Arusha zinatarajiwa kupokea msaada wa ngo’mbe 500, baada ya kukumbwa na ukame uliokumba maeneo ya malisho ya familia hizo mwaka 2009.


Ahadi hiyo iliyoanza kutekelezwa tangu Februari, 2012 na Rais Jakaya Kikwete katika wilaya ya Longido, sasa inaelekezwa katika wilaya hiyo na Rais Kikwete ndiye anatarajiwa kuwakabidhi wafugaji hao. 

Tukio hilo ambalo huvuta hisia za wafugaji wengi linatarajiwa kuwakutanisha viongozi mbalimbali wa maeneo hayo, akiwamo Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa na Saning”o ole Telele wa Ngorongoro. 

Akizungumzia sherehe hizo zinazotarajiwa kuanzia leo wilayani Monduli, Mkuu wa wilaya hiyo, Jowika Kasunga, alisema wafugaji watakaonufaika na msaada huo ni wale waliopoteza ng’ombe wao wakati wa ukame mkali ulioyakumba maeneo ya wafugaji hao katika mwaka 2009 na kusababisha maelfu ya mifugo ikiwamo ng’ombe na mbuzi kufa kwa kukosa malisho na maji. 

“Ugawaji huo wa mifugo hii ni muendelezo wa mradi wa ugawaji wa mifugo kwenye wilaya tatu za Monduli, Ngorongoro na Longido. Kama utakumbuka tayari Wilaya ya Ngorongoro ilishakabidhiwa mifugo 11,000 ya wananchi wake Februari mwaka huu,” alisema Kasunga.

Alisema Rais Kikwete atagawa mifugo 500 kwa familia 125 za wilayani humo, ambapo kila familia inayohusika inatarajiwa kufaidika na mifugo minne. Baadaye ugawaji wa ng’ombe na mbuzi wengine wapatao 6,000 kwa familia 1,400 utaendelea wilayani Monduli.

Akizungumzia kuhusu ugawaji wa mifugo hiyo katika Wilaya ya Ngorongoro, alisema mpango huo utafanyika katika Kata ya Loliondo ambako jumla ya mifugo
7,400 itagawanywa kwa familia 1,850.

Katika ukame huo uliotokea mwaka 2009 takriban mifugo 700,000 ilikufa kwa njaa, kutokana na kukosa malisho na maji ya kunywa.

Kuendelezwa kwa ahadi hiyo sasa kunafanya ahadi hiyo kufikia kiasi cha Sh bilioni 11.2 kwa wilaya tatu ambazo ni Ngorongoro, Longido na Monduli.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa