Arusha
Home » » MAGUFULI AMTAKA MKURUGENZI TANROADS KUKOMESHA RUSHWA

MAGUFULI AMTAKA MKURUGENZI TANROADS KUKOMESHA RUSHWA


Idd Uwesu, Arusha
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Patrick Mfugale, kukomesha vitendo vya rushwa vilivyokithiri katika kitengo cha mizani vinavyofanywa na wafanyakazi wasio waaminifu na kusababisha uharibifu mkubwa wa barabara.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana, wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa wadau wa Bodi ya Barabara.

Alisema asilimia 80 ya wafanyakazi wa mizani hapa nchini ni wala rushwa wakubwa na kusababisha idadi kubwa ya barabara kuharibika vibaya kutokana na kuruhusu magari yenye ujazo mkubwa kupita.

“Asilimia 80 ya wafanyakazi wa mizani ni wala rushwa wakubwa, nakuagiza mkurugenzi hakikisha unafanya uchunguzi wa kina na uhakikishe rushwa inakomeshwa.

“Tumekuwa tukituma watu wetu kuchunguza tuhuma hizo, lakini cha ajabu nao walikuwa wakiingia katika mkumbo wa kupokea rushwa, hii ni hatari, sasa tumia mbinu nyingine hadi vitendo hivyo vikome,’’ alisema Dk. Magufuli.

Aidha, alimtaka kuhakikisha anawatimua kazi mara moja wafanyakazi wasio waadilifu bila kujali wameingizwa na waziri ama kigogo yeyote mwenye cheo kikubwa, kwa kuwa hali hiyo inachangia kuwapo kwa ufanisi mdogo wa utendaji kazi katika mizani.

Alitolea mfano Barabara ya Chalinze hadi Morogoro ambayo imeharibika kwa kulalia upande wa kushoto kutokana na magari yanayotokea Dar es Salaam kuelekea Morogoro kupita na uzito mkubwa bila kuchukuliwa hatua na kufanya barabara hiyo kulalia upande mmoja.

Alizionya halmashauri zote nchini kuacha mara moja kubadilisha matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara na kuzielekeza katika matumizi mengine, ikiwamo kulipana posho za vikao, ununuzi wa vitafunio, matengenezo ya magari na ununuzi wa vifaa vya ofisi.

Alitolea mfano Halmashauri  za Morogoro, Chato, Kigoma, Biharamulo, Misenyi, Dodoma, Kishapu, Mafia, Mwanga, Geita, Musoma, Kibondo, Njombe, Bariadi na Tarime kuwa zimetumia vibaya fedha za mradi wa barabara kwa kuelekeza katika matumizi mengine.

Alitaka Bodi ya Mfuko wa Barabara kuhakikisha inasimamia ipasavyo matumizi ya fedha za barabara, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wakandarasi wanaopewa zabuni za ujenzi wa barabara na miradi ya barabara kutokamilika kwa wakati.

Hata hivyo, alisema jumla ya barabara za lami hapa nchini zenye urefu wa kilomita 11,154 zimetengenezwa  na hadi kufikia mwaka 2015, jumla ya barabara zenye urefu wa kilomita 17,500 zitatengenezwa na kufanya Tanzania iwe miongozi mwa nchi tano za Afrika zenye mtandao wa barabara za lami.

Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa