Arusha
Home » » LOWASSA: RAIS KIKWETE NI JASIRI, MWADILIFU

LOWASSA: RAIS KIKWETE NI JASIRI, MWADILIFU

Na Mwandishi Maalumu, Monduli
WAZIRI Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, amemweleza Rais Jakaya Kikwete kuwa ni rais wa kwanza katika historia ya Tanzania kujali wafugaji kwa kiasi kikubwa mno na kiongozi mwenye uwezo wa kuchukua uamuzi wa kijasiri, kishujaa na kwa uadilifu.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa juzi, wakati alipozungumza katika sherehe ya kukabidhi ng’ombe kwa wananchi wa Wilaya ya Monduli waliopoteza mifugo yao kutokana na ukame uliolikumba eneo la kaskazini mwa Tanzania mwaka 2008/2009.

Lowassa, aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Rais Kikwete kati ya 2005 na 2008, aliwaambia wananchi waliohudhuria sherehe hizo: “Nimesimama kukushukuru Mheshimiwa Rais kwa msimamo wako wa kutetea wafugaji wa Tanzania. Hakuna Rais yeyote katika historia ya nchi yetu amepata kuwajali na kuwatetea wafungaji wa Tanzania kama wewe.

“Nakupongeza kwa uamuzi wako wa kishujaa, kijasiri na wenye kuongozwa na uadilifu, kama huu uamuzi wako wa kutoa kifuta jasho kwa wananchi wetu ambao walipoteza mifugo yao yote wakati ule wa ukame.”

Aidha, amempongeza Rais Kikwete kwa uamuzi wake wa kutoa kiasi cha Sh bilioni tatu za kukarabati mabwawa na madaraja yaliyoharibiwa na mvua kubwa iliyofuatia miaka ya ukame.

“Mheshimiwa Rais, kama unavyojua mvua ile kubwa iliyofuatia ukame mkubwa iliharibu sana mabwawa na madaraja yetu na nikaomba msaada wako. Nilikushuhudia wewe mwenyewe ukitoa maelekezo kwa Waziri Mkuu kuwa sisi Monduli tupewe fedha hizo na nashukuru sana tumepata,” alisema Lowassa.

Aidha, amemshukuru Rais Kikwete kutokana na Wilaya ya Monduli kupewa fedha za kuendeleza elimu wilayani humo kutokana na fedha iliyorudishwa na Serikali ya Uingereza kwa Serikali ya Tanzania kutokana na ununuzi wa rada.

“Nikushukuru pia kutokana na ule mgawo kutokana na rada change. Tumepokea fedha na tumezitumia kukarabati shule mbili za sekondari wilayani kwetu. Tunakushuru sana Mheshimiwa Rais,” alisema Lowassa.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa