Na Eliya Mbonea, Arusha
SABABU za kushuka kwa elimu nchini zimetajwa kuchangiwa na kuwapo kwa idadi kubwa ya wanafunzi ndani ya darasa moja.
Hayo yalibainika mjini hapa juzi wakati wa mjadala wa wazi uliofanywa baada ya kukamilika kwa Utafiti wa Marafiki wa Elimu mkoani Arusha ukiwa umesimamiwa na Shirika la Haki Elimu.
Akizungumza katika mjadala huo, Josephine Shayo, kutoka kundi la marafiki hao wa elimu, alisema changamoto zinazofanya kushuka kwa elimu ambazo alizitaja baadhi kuwa ni wingi wa wanafunzi ndani ya darasa moja.
Alisema katika utafiti walioufanya katika shule sita za msingi na sekondari tatu ndani ya Halmashauri ya Arusha iliyopo wilayani Arumeru, ambapo waliweza kubaini changamoto hizo.
“Tumekuta darasa moja linakuwa na wanafunzi 127, ambao hujikuta wakifundishwa na mwalimu mmoja badala ya wanafunzi 40 wa shule za awali.
“Hali hii tupende tusipende lazima itazalisha watoto wasiojua kusoma wala kuandika ambao hupelekwa shule za msingi,” alisema Josephine.
Aliitaja changamoto nyingine iliyobainishwa katika mjadala huo wa wazi ilikuwa ni ukosefu wa nyumba za walimu, ambapo baadhi ya shule kama Shule ya Msingi Engorika iliyoko Kijiji cha Olkokola, wilayani humo ikiwa na walimu 12 wanaoishi nyumba moja.
“Pia kumekuwapo na waalimu wasiopenda kazi zao kama miaka ya nyuma, hali inayosababisha Serikali kuajiri waalimu wasio na sifa na kusababisha kushuka kwa elimu,” alisema Josephine.
Naye, Ofisa Programu Idara ya Uongozi wa Kimkakati, Ofisi ya Haki Elimu, Elisante Kitulo, alisema mjadala huo uliandaliwa baada ya kukamilika utafiti katika Shule za Msingi ya Engorika, Olasiva, Umoja na Naurei.
Alisema kwa upande wa shule za sekondari, alizitaja kuwa ni Mateves, Onyoito na Kimnyaki.
“Katika shule hizi tumegundua miundombinu ya elimu ni mibovu na inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa, kwa ajili ya kuboresha elimu kwa lengo la kupunguza kushuka kwa elimu nchini,” alisema Kitulo.
Alisema Shirika la Haki Elimu limekuwa likifanya kazi kupitia marafiki hao katika wilaya 10.
Alizitaja wilaya hizo kuwa ni Ukerewe, Iramba, Arusha, Serengeti, Bariadi, Tabora, Kilwa, Kilosa, Kigoma Vijijini na Muleba.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment