Na Idd Uwesu (Arusha yetu Blog)
Wabunge wa bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki wameapishwa rasmi jijini Arusha tayari kwa kuanza kazi katika Bunge la tatu la jumuiya hiyo mara baada ya bunge la pili kumaliza muda wake.
Sherehe za kuwaapisha wabunge hao zimefanyika kwenye ukumbi wa bunge hilo katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Arusha AICC jijini humo.
Shughuli za kuwaapisha wabunge hao zilianza kwa mchakato wa kumpata Spika wa Bunge hili ambapo ikiwa ni zamu ya nchi ya Uganda kutoa Spika, wabunge hawa ilibidi kufanya uchaguzi ambapo Mh. Margareth Ziwa aliibuka mshindi wa kiti hicho kwa kumshinda Mh. Byamukama kwa kura 33 kwa 12 ikiwa ni duru ya pili ya uchaguzi huo mara baada ya kushindwa kufikia wastani wa theluthi tatu ya kura zote zinazostahili mgombea kuzipata katika duru ya kwanza.
Mh. Ziwa anakuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki akichukua nafasi iliyoachwa na Mh. Abdirahim Abdi kutoka Kenya.

0 comments:
Post a Comment