Home » » Vigogo CCM, Chadema Wahojiwa Polisi Arumeru

Vigogo CCM, Chadema Wahojiwa Polisi Arumeru





Waandishi Wetu, Arumeru
BAADHI ya viongozi wa vyama vyenye upinzani mkubwa katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki wamehojiwa na polisi kutokana na kuwepo kwa vitendo kadhaa vya uvunjifu wa amani.
Viongozi waliokamatwa na polisi wakihusishwa na vurugu za vyama vyao na kuhojiwa ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Ndengaso Ndekubali na Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Allan Kingazi.

Kukamatwa kwa viongozi hao kumekuja siku moja tangu Kamati ya Maadili ya vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo kutoa onyo kwa CCM na Chadema kutokana na kuhusika kwake na vitendo vya ukiukwaji wa maadili kwenye uchaguzi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia Msimamizi wa Uchaguzi huo, Trasias Kagenzi alisema pamoja na vyama hivyo kupewa onyo masuala mengine yaliachwa ili kutoa fursa kwa polisi kuyafanyia kazi kwani yalihusisha moja kwa moja uvunjaji wa sheria za nchi.

Mkuu wa Oparesheni ya Polisi katika uchaguzi huo, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu alisema viongozi hao wamehojiwa kutokana na kulalamikiwa kwa tuhuma tofauti za uvunjifu wa amani katika uchaguzi huo.

Alisema Mchungaji Msigwa alihojiwa kutokana na kutuhumiwa na CCM kuhusika katika fujo zilizofanywa na wafuasi wa Chadema katika eneo la Meru Garden Machi 17, mwaka huu ambako msafara wa mgombea ubunge wa CCM, Sioi Sumari ulishambuliwa kwa mawe na gari moja lilijunjwa kioo.

Kuhusu makatibu wa CCM, Kamanda Mngulu alisema walihojiwa kutokana na kutajwa kuhusika na tukio la kumteka nyara, Mwenyekiti wa Chadema Kitongoji cha Magadilisho, Nuru Maeda (53), kumpiga kisha kumtesa kwa kumvuta korodani, tukio ambalo linadaiwa kutokea asubuhi ya Machi 19.

“Tumewakamata na tumewahoji na kuwaachia kwa dhamana wote na upelelezi ukikamilika tutawafikisha mahakamani,” alisema Mngulu.

Dk Slaa, Shigela waonywa
Katika hatua nyingine, DCP Mngulu amewaonya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Martin Shigela kuacha kutoa lugha za uchochezi kwenye kampeni.

Kauli hizo ni zile zilizotolewa na Dk Slaa juzi pale alipowapa polisi saa 24 ili wawakamate mara moja viongozi wa CCM waliohusika na utekaji wa kiongozi wa Chadema na kusema kwamba haki isipotendeka katika uchaguzi huo, Arumeru itakuwa eneo la kwanza kuanzisha maandamano hadi Ikulu.

Kwa upande wa Shigela, alinukuliwa akisema kushambuliwa kwa msafara wa mgombea wa CCM Machi 17 ni tukio la mwisho na kamwe hawatavumilia na kama polisi hawatachukua hatua, basi vijana wa chama hicho wataingia msituni.
Mngulu alisema kauli hizo hazikubaliki na kwamba viongozi hao wanakiuka sheria hivyo kuwaonya kwamba hawawezi kuwafundisha polisi jinsi ya kutekeleza wajibu wao.

Mngulu alisema kitendo Dk Slaa kuwapa polisi saa 24 ni uchochezi unaoweza kusababisha kuvunjika kwa amani na kumwambia ikiwa anataka kuwa polisi, basi aachane na siasa ili ajiunge na jeshi hilo.

Hata hivyo, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kiwawa jana, Dk Slaa alisema Chadema wamechoka kuonewa na polisi, huku akilaani kile alichodai kuwa ni kukamatwa ovyo kwa viongozi na wafuasi wa chama hicho.
“Naomba mumweleze huyu Mngulu kuwa tumechoka kunyanyaswa, wamepiga vijana wangu Kiteto, Tarime, Busanda, Biharamulo na Igunga ambako Mngulu pia alikuwa mkuu wa operesheni na hakuna hatua zilizochukuliwa, badala yake vijana wa Chadema ndiyo wanafunguliwa kesi na baadaye kesi zinafutwa,” alisema Dk Slaa na kuongeza:

“Mimi sina shida na nyie vijana wadogo wa polisi kwani mnatumwa tu, lakini hawa wakubwa tunawataka waache kutumiwa na CCM wafanye kazi ya kulinda raia na mali zao na siyo kazi ya kuilinda CCM.”

Kwa upande wake, Meneja Kampeni mwenza wa Chadema, Vicent Nyerere aliwataka maofisa wa usalama wa Taifa ambao wamekuwa wakifuatulia mikutano na Chadema kuacha kutumiwa na CCM kwani kazi yao ni kulinda usalama wa Taifa.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara Kijiji cha Kiwawa, Kata ya Maji ya Chai, Nyerere ambaye ni Mbunge wa Musoma Mjini alisema ni aibu kwani wakati madini ya tanzanite yanatoroshwa nchini maofisa hao wapo wakihangaika na Chadema.Soma zaidi 

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa