[Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa]
LASEMA KAMA ANAO USHAHIDI WA WIZI WA FEDHA ZA PAPA AUTOE, WANASIASA WANAOCHAFUA WENZAO WAMEFILISIKA, NEC YAVIONYA CCM, CHADEMA
Na Waandishi Wetu
KANISA Katoliki nchini limemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano wa Jamii), Stephen Wassira kutoa ushahidi kuthibitisha kama Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alifukuzwa upadre baada ya kuiba fedha za ujio wa Papa John Paul II, alipokuja nchini mwaka 1991.Akizungumza kwa simu jana, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec), Yuda Thadeus Ruwaichi alimtaka Wassira athibitishe tuhuma zake akisema kanisa hilo halijawahi kumtuhumu Dk Slaa kwa tuhuma za wizi.
Akizungumza katika kampeni za CCM Jimbo la Arumeru Machi 19, mwaka huu, Wassira alimtupia kombora Dk Slaa akidai si mwaminifu kwa kuwa alifukuzwa ukasisi wa kanisa hilo baada ya kufanya ufisadi kwenye fedha za mapokezi ya Papa huyo ambaye sasa ni marehemu.
Hata hivyo, Wassira jana alipotakiwa kuzungumzia kauli hiyo ya Askofu Ruwaichi alijibu kwa kifupi: “Mimi nilishazungumza na yakaandikwa kwenye vyombo vya habari, hii leo siyo habari.”
Ruwaichi ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza alisema madai hayo ya Wassira hayana msingi.
“Kanisa halijawahi kumshutumu Dk Slaa kuhusu madai hayo (ya Wassira). Kama Wassira ameyatoa kwenye mkutano wa hadhara, njia sahihi ya kupata ukweli ni yeye kutupa ushahidi wa vielelezo kuthibitisha madai yake,” alisema Ruwaichi.
Askofu Ruwaichi amewaonya wanasiasa wanaofanya kampeni za kuchafuana akiwataka waache na waanze kufanya siasa za kistaarabu.
“Ukiona mwanasiasa anakurupuka na kuanza kumchafua mwenzake ujue amefilisika, vitendo hivyo vinaonyesha udhaifu kwa nchi katika nyanja za siasa,” alisema.
Askofu Ruwaichi alisema wanasiasa waliokomaa hawapaswi kufanya kampeni za kuchafuana... “Watajishughulisha katika kujadili hoja zinazozingatia mahitaji ya jamii. Kitendo cha wanasiasa wetu kufanya kampeni za kuchafuana kinaonyesha dhahiri kuwa bado tuko dhaifu katika siasa na hatuna vipaumbele.”
Askofu Ruwaichi aliwataka wanasiasa hao kuachana na kampeni chafu na badala yake wajikite katika kujadili hoja zinazotoa vipaumbele katika matatizo yanayoikabili jamii na namna ya kuyatatua ili kuwawezesha wananchi kuchagua viongozi bora.
Kauli hiyo ya Askofu Ruwaichi, imekuja siku chache baada ya Dk Slaa kuzungumza katika mkutano wa hadhara kwenye kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru na kusema Wassira ni mwongo na hajui asemalo.
“Kama tangu mwaka 1991 nipo, basi kitendo cha Serikali kushindwa kunifungulia mashtaka ya wizi wa hizo fedha basi ni Serikali dhaifu na ijiuzulu,” alisema Dk Slaa.Soma zaidi www.mwananchi.co.tz
0 comments:
Post a Comment