Arusha
Home » » UNESCO yajiandaa kutoa tamko zito urithi wa

UNESCO yajiandaa kutoa tamko zito urithi wa

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.
MACHO na masikio ya nchi zote duniani yameelekezwa Tanzania wiki hii ambako imetangazwa kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) inatarajia kutoa tamko zito.
Tamko hilo la Unesco linalosubiriwa kwa shauku kubwa, kama sio hofu na nchi nyingi duniani litatolewa rasmi siku ya Jumamosi ijayo wakati viongozi wake watakapokuwa katika moja ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyomo nchini yaani Hifadhi ya Ngorongoro iliyopo wilayani Ngorongoro mkoani hapa.
Mkurugenzi Mkuu wa Unesco, Dk Mechtild Rossler ambaye yuko mjini Arusha kuhudhuria Mkutano Mkuu wa masuala ya ‘Urithi wa Afrika,’ na nafasi yake katika maendeleo ya jamii, alisema wanatarajia kuhitimisha mkutano huo wa siku tano kwa kufanya kikao maalumu cha maamuzi katika Bonde la Ngorongoro mwishoni mwa wiki, ambako wanatarajia kutoa tamko kuu rasmi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefungua rasmi mkutano huo unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) jijini Arusha jana huku akitilia mkazo umuhimu wa kuyalinda na kuyahifadhi maeneo muhimu nchini yakiwemo yale yaliyopewa hadhi ya urithi wa dunia na taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa.
“Tunaelewa kwamba utunzaji wa maeneo ya urithi wa dunia unagubikwa na matatizo mengi, likiwemo suala la mabadiliko ya tabia ya nchi, ongezeko la watu na mifugo na vile vile migogoro ya ardhi katika nchi nyingi barani Afrika,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aliwaomba washiriki wa mkutano huu wa Unesco kuja na suluhisho la jinsi ambavyo vivutio vya asili pamoja na maeneo ya urithi wa dunia ambayo pia yana madini muhimu yanavyoweza kutunzwa pamoja na nchi nyingi kuwa na uhitaji mkubwa wa vito vya thamani vipatikanavyo humo.
Pori la Akiba la Selous mkoani Iringa ambalo pia ni moja ya maeneo saba ya Urithi wa Dunia, liliwahi kukumbwa na changamoto kama hiyo baada ya kugundulika madini ya urani.
Pamoja na nchi kadhaa kushiriki mkutano wa Unesco, bado nyingine nyingi duniani zimeelekeza macho na masikio yao Tanzania ambako ndiko tamko la Unesco linatarajiwa kutolewa wiki hii, huku ikiwa haijulikani litahusisha kitu gani ingawa baadhi wanahofia kuwa pengine baadhi ya maeneo ya urithi wa dunia yakafutwa rasmi Jumamosi.
Hadi sasa, Unesco imeyaorodhesha maeneo 1,031 duniani kama ‘Maeneo Maalumu ya Urithi wa Dunia huku Italia ikiongoza kwa kuwa na sehemu nyingi zaidi (51), ikifuatiwa na China (48), Hispania (44), Ufaransa (41), Ujerumani (40), Mexico (33) na India (32).
Bara la Afrika lina sehemu 91 zilizoainishwa na Unesco kama maeneo ya Urithi wa Dunia na saba kati ya hizo, zinapatikana Tanzania; ambayo ni Bonde la Ngorongoro, Hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Mji Mkongwe wa Unguja, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, Michoro ya Mapango ya Kolo, Kondoa na Pori la Akiba la Selous.
“Na ni kutokana na uhifadhi bora katika Tanzania ndio maana mkutano huu mkubwa wa kimataifa unafanyika nchini,” alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Chanzo Gazeti La Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa