Na Eleuteri Mangi-
Arusha.
16/12/2014
Serikali ya Tanzania
inaendelea vema na mpango wake wa kutoa elimu ya msingi kwa watoto wote waliofikia
umri wa kwenda shule nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa wakati akiwasilisha mada
yake inayohusu “Namna Tanzania inavyoboresha Usawa wa Kinga ya Jamii katika
sekta ya elimu” katika kongamano la kimataifa linaloendelea katika siku ya pili
jijini Arusha kuhusu Kinga ya Jamii.
Dkt. Kawambwa alisema
kuwa mpango huo unaanzia elimu ya awali, shule ya msingi na sekondari ambapo
kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule apate elimu ambayo ndiyo msingi wa kinga
ya jamii nchini tofauti na awali ambapo elimu ya msingi ilikuwa kwa watoto
wenye umri kuanzia miaka 7 hadi 14.
Dkt. Kawambwa
alisisitiza kuwa mpango huo wa kinga ya jamii nchini unaenda sanjari na Mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao Tanzania imeanza kuutekeleza mwezi Aprili,
2013 ambapo unatarajiwa kuhitimishwa 2017.
Ili kufikia malengo ya
kuboresha mpango wa kinga ya jamii nchini, Dkt. Kawambwa aliwaambia wajumbe wa
kongamano hilo kuwa mbinu zinazotumiwa na Tanzania katika kutekeleza mpango wa
BRN na kuboresha kinga ya jamii ni pamoja na kuboresha vifaa vya kujifunza na
kufundishia shuleni, kusimamamia mpango wa wanafunzi kujua kusoma, kuandika na
kuhesabu na kuboresha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya ndani na ya taifa.
Mbinu nyingine ni kuwapa
motisha walimu, kutoa motisha kwa shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya taifa kwa shule
zote iwe ya msingi au sekondari na kuwawezesha walimu na wanafunzi kujua wajibu
wao kwenye sekta ya elimu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa ufanisi ili
kuongeza nguvu kazi ya wataalam ambao ndio msingi wa kuboresha kinga ya jamii
na hivyo kupunguza tatizo la umaskini nchini.
Aidha, Dkt. Kawambwa
alisema kuwa viashiri ambavyo vinaonesha Tanzania inaendelea kupata mafanikio
katika kuimarisha sekta ya elimu na kuimarisha kinga ya jamiina ni pamoja na
kuongezeka ufaulu katika mitihani ya taifa ambapo mwa 2013 ufaulu kwa shule za
msingi na sekondari ulikuwa zaidi ya asilimia 60, mwaka 2014 kwa asilimia zaidi
ya 70 na inatarajiwa 2015 ufaulu huo utaongezeka kufikia asilimia 80.
Akijibu swali la Katibu
Mkuu Wizara ya Kazi, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Huduma Ali N. Ismail kutoka
Kenya aliyetaka kujua kwanini Tanzania bado inatumia mpango wa kupanga shule
katika madaraja ambao unaweza kupunguza morali kwa baadhi za shule ambazo
inaweza kuwa chanzo cha kupunguza
uwezekano wa kutoboresha mpango wa Kinga ya jamii.
Dkt. Kwambwa alisema
kuwa Serikali inasimamia mpango huo kwa kuwahusisha wanafunzi wote na shule
zote bila kubagua na kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, walimu wamepata
mafunzo ambayo yanawawezesha walimu hao kusimamia wanafunzi wenye mahitaji
maalum kulingana na hali zao na amesema Tanzania ipo tayari kujifunza kutoka
Kenya namna wanavyofanikiwa kuacha na mpango wa kupanga shule katika madaraja.
Kwa upande wa wanafunzi
wenye ulemavu wa ngozi, Waziri Kwawambwa alisema kuwa kwenye suala la mitihani wanafunzi
hao wamepewa kipaumbele kwenye suala la muda ambapo wao huongezewa baada ya
muda wa kawaida wa mtihani kuisha na mitihani yao imeandikwa kwa maandishi
makubwa zaidi ili kuwasaidia kusoma vizuri zaidi.
Kongamano la kimataifa
linalohusu Kinga ya Jamii linaloendelea jijini Arusha limeandaliwa na Serikali
ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha, Idara ya Kuondo Umaskini kwa kushirikiana
na UNICEF, ILO, UNAIDS na EPRI ambapo washiriki wa konngamano hilo wanatoka
katika nchi za Kenya, Uganda, Bangladesh, Afghanistan, Msumbiji, Lesotho,
Malawi, Afika Kusini, Ghana, Ethiopia, Zambia, Sudani kusini na mwenyeji
Tanzania.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment