Arusha
Home » » POLISI YAINGILIA MAJUKUMU YA LEMA

POLISI YAINGILIA MAJUKUMU YA LEMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
HATUA ya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya wabunge wa upinzani majimboni kwao kwa kisingizio kwamba inagongana na ile ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemwibua Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) na kumtaka mkuu wa polisi wilayani hapa (OCD), Gires Muroto kuacha kufanya kazi kwa maelekezo ya kisiasa badala yake asimamie sheria na kanuni.
Lema alisema hatua ya OCD huyo kufuta mikutano yake ya kibunge aliyokuwa ameiruhusu kwa kigezo kuwa amepokea maombi mengine ya CCM ya kufanya mikutano kwenye maeneo aliyokuwa amemruhusu kufanya mikutano ni ya ubabaishaji.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, Lema alisema kuwa Aprili 17, mwaka huu, alimwandikia barua OCD akiomba kufanya mikutano ya wananchi kwa nafasi yake kama mbunge kwenye kata za Levelosi, Terrat, Daraja Mbili na Moshono kwa tarehe tofauti.
Alisema kuwa siku hiyo hiyo alipokea barua toka kwa OCD akimruhusu kuendelea na mikutano yake, lakini katika hali isiyo ya kawaida, Aprili 20 akapokea barua nyingine kutoka kwa kiongozi huyo akizuia mikutano hiyo.
“Sababu alizozitoa OCD hazina mashiko, mimi ni mbunge wa wananchi wote wa Arusha, wakiwemo CHADEMA na CCM, hata Mary Chatanda (Katibu wa CCM Mkoa) mimi ni mbunge wake, hivyo nilipompa taarifa OCD alipaswa kuelewa kuwa naenda kuzungumza na wananchi wote wa Arusha, si wa chama changu pekee, hivyo kuzuia mikutano yangu eti kwa sababu siku mbili baadaye CCM wameomba kufanya mikutano si sahihi.
“OCD amekuwa akitumia sababu hii kuzuia hata mikutano ya CHADEMA. Mtakumbuka wakati ule wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Kata ya Sombetini, maandamano ya CHADEMA kupinga uonevu wa CCM na polisi yalizuiwa kwa kigezo kuwa CCM nao wanataka kuandamana,” alisema Lema.
Alisema kuwa hoja ya pili aliyotoa OCD kuzuia mikutano yake kuwa wanazuia mikusanyiko, hasa baada ya bomu lililotokea kwenye baa ya Arusha Night Park nayo haina ukweli kwani watu wameendelea kukusanyika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha ikiwemo baa, sokoni kwenye kumbi za starehe na zile za ibada.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na OCD Muroto yenye kumbukumbu namba AR/B.5/Vol.III/162 ambayo Tanzania Daima inayo nakala yake, kiongozi huyo anakiri kupokea barua ya Lema na kuwa alimruhusu kuendelea na mikutano, lakini anaizuia kwa sababu CCM nao wameomba mikutano maeneo hayohayo na tarehe hizohizo.
“Itakuwa sio busara kuruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama viwili vinavyopingana kisera, maudhui na mtazamo kufanya mikutano katika maeneo, muda na siku zinazofanana kwani inaweza kupelekea uvunjifu wa amani wakati wa mikutano hiyo.
“Hivi karibuni kumetokea tukio la mlipuko wa bomu… tukio hilo limeleta hofu kwa wananchi na bado limo katika mawazo ya watu, haitakuwa busara kuendelea kuruhusu mikusanyiko bila kutoa kipaumbele cha kuimarisha usalama, kwa mantiki hiyo Jeshi la Polisi tumeelekeza nguvu zetu katika kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya Jiji la Arusha,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa