Arusha
Home » » WENYE VIWANDA WATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI WAO

WENYE VIWANDA WATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI WAO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

SERIKALI imewataka wenye viwanda nchini kuongeza kasi ya uzalishaji bidhaa ili kutumia fursa ya soko kubwa la ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji tuzo za Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) mwishoni mwa wiki Waziri wa Viwanda na Biashara, Abdallah Kigoda alisema hali inavyojionesha sasa inatabiri mwelekeo wa ushindani mkubwa katika kuendeleza viwanda toka nchi jirani ambazo zinalenga kutumia fursa za masoko ya ndani na nje ya utaratibu bila ushuru na bila kikomo (DFQF).
Alisema, Wizara kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) inaendelea kutenga maeneo ya EPZ na SEZ kama moja ya mikakati ya kuvutia uwekezaji na kuongeza uzalishaji viwandani ili kukuza ajira.
Aliongeza kuwa, mpaka sasa maeneo haya yametoa ajira kwa wafanyakazi 26,381 hadi kufikia Juni 2013 na ajira hizo zinatarajia kuongezeka kadri viwanda zaidi vitapoanza uzalishaji.
Alisema, kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa viwanda 13 vimepewa vibali chini ya utaratibu huu.
Vilevile Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linaendelea na jitihada za kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ya kuanzisha viwanda mama ambayo inatekelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Mwenyekiti wa (CTI), Dkt. Samuel Nyantahe aliiomba serikali kuhimiza Mamlaka ya Bandari (TPA) kuongeza ufanisi wa miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam kwa kuongeza winchi za kupakulia mizigo bandarini kwani zilizopo hazitoshelezi.
Pia aliiasa serikali kuharakisha mpango wake wa kuweka bandari kavu Kisarawe na kuimarisha reli ya kuchukua mizigo kutoka bandarini ili kupunguza msongamano wa mizigo kukaa bandarini kwa muda mrefu.
Alisema, hakuna mabehewa na injini za treni za kutosha hali inayosababisha mizigo mingi mizito kusafirishwa kwa barabara, usafiri ambao ni wa gharama kubwa na huchangia barabara kuharibika baada ya muda mfupi.
Aliongeza kuwa, pamoja na matatizo mengi sekta ya viwanda imefanya vizuri kwa kuongeza mauzo ya bidhaa za viwandani nje ya nchi.
Alisema mauzo ya nje yaliongezeka kutoka dola za Kimarekani milioni 861.5 mwaka 2011 na kufikia dola za milioni 1,047.3 mwaka 2012.
Alisema, hilo ni ongezeko la asilimia 21.6.
Mwenyekiti huyo alisema, mauzo ya bidhaa za viwandani yalichangia asilimia 25 ya thamani ya mauzo yote Tanzania nchi za nje.
"Tunategemea kuwa sekta ya viwanda itaendelea kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi yetu,ikiwa ni pamoja na kuipatia serikali mapato yake kutokana na kodi na tozo mbalimbali,"alisisitiza.
Alisema pamoja na mafanikio hayo katika sekta ya viwanda kwa mwaka 2013 mafanikio hayo ni madogo ukilinganisha na uwezo na fursa zilizopo.
Dkt.Nyantahe alisema, katika kusimamia biashara kwenye mfumo wa soko huria, serikali ilianzisha taasisi za usimamizi na udhibiti wa biashara ili kudhibiti mwenendo wa kibiashara na kuwalinda walaji.
Alisema taasisi nyingi zilizoanzishwa zinafanya kazi zinazofanana hivyo kuongeza urasimu na muda katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, taasisi hizo zimekuwa zikiwatoza wafanyabiashara ada kubwa ili ziweze kugharamia shughuli zake za kiutendaji hali inayosababisha kuongeza gharama za kufanya biashara.

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa