TANZANIA na Rwanda zinazidi kufanya vizuri katika ubunifu na ujenzi
wa viwanda vya kisasa ambapo sasa zinatengeneza na kuuza nje magari ya
kubeba watalii, malori ya taka na pikipiki.
Kampuni ya Pikipiki Rwanda (RMC) jijini Kigali iliyoanza kutengeneza
aina mbalimbali za pikipiki kuanzia katikati ya mwaka huu, imekuwa gumzo
na bidhaa zake zimeanza kuvutia wafanyabiashara wa Tanzania, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na nyingine.
Aidha, Kampuni ya Hanspaul Automechs Limited (HAL) iliyo eneo la
viwanda Njiro jijini Arusha imekuwa gumzo kwa kutengeneza magari makubwa
ya kubeba watalii maarufu kwa jina la ‘War Bus’ ambayo Mkurugenzi wa
kampuni hiyo, Satbir Hanspaul amesema yanauzwa Kenya, Afrika Kusini na
Ulaya pia. PIKIPIKI ZA RWANDA Mkurugenzi wa Mauzo wa Kampuni ya RMC,
Luois Masengesho anasema wafanyabiashara mbalimbali wa Tanzania na DRC
tayari wamewasilisha maombi kununua pikipiki zao.
“Hadi sasa tumekuwa tukiuza pikipiki kwenye soko la Rwanda lakini
watu kutoka Tanzania na DRC wameonesha nia ya kuzinunua,” alisema.
Kiwanda hicho kiko Ukanda Maalumu Kiuchumi na kilifungua duka la kuuza
pikipiki Mei 2017. Masengesho alisema, hadi sasa kimetengeneza zaidi ya
pikipiki 300, na 130 kati ya hizo zimeshauzwa kwenye soko la Rwanda.
RMC inatengeneza aina saba za pikipiki Ingenzi, Indakangwa,
Indahigwa, Imparage, Infarasi na Inzovu na kila moja inauzwa kati ya
Faranga za Rwanda milioni 1.2 hadi Faranga milioni 3 kwa kuzingatia
uwezo wa injini na ukubwa wake zikiwemo za CC250 na CC125. Masengesho
amesema walengwa wakubwa wa pikipiki hizo ni wafanyabiashara wa
bodaboda, wanaozitumia kwa ajili ya michezo, maofisa wa Serikali na
mashirika yasiyo ya kiserikali huko.
“Tunashukuru soko limetupokea vizuri na kwa sababu ya mahitaji
yaliyoonekana katika nchi hizi (Tanzania na DRC) tunatarajia kuongeza
mauzo zaidi na zaidi,” alisema Masengesho. Alisema baadaye mwezi huu
pikipiki hizo zinatarajiwa kuwa kivutio kwenye maonesho ya kila mwaka ya
bidhaa zinazozalishwa Rwanda. MAGARI YA TANZANIA HAL imesema imebuni na
kutengeneza magari maalumu ya kubeba takataka yanayofaa kwa mazingira
ya Tanzania na Afrika Mashariki, ikiwemo hali ya hewa, barabara na mfumo
wa maisha na hivyo yatadumu kwa muda mrefu.
“Lakini aina mpya ya malori ya kubeba takataka si kwa ajili ya
kampuni yetu au kiwanda chetu tu. Kwa kuzingatia viwango vya TBS
(Shirika la Viwango Tanzania), wazalishaji wengine pia wanaweza
kutengeneza wakitumia utambulisho wa ubunifu wa HAL kama kielelezo,”
alisema Mkurugenzi wa HAL, Hanspaul.
Alisema magari ya kubeba takataka na yale ya watalii ni ubunifu wa
Tanzania unaozivutia nchi nyingine zikiwemo za Ulaya na magari ya
watalii yanayokubalika soko la kimataifa. “Watu wengi hawataamini nchi
zenye viwanda vya kutengeneza magari kama Afrika Kusini na zile za Ulaya
sasa zinanunua magari kutoka Tanzania, lakini wanafanya hivyo,”
alisema.
Magari hayo yenye nembo za Toyota, Nissan na Land Rover
yanatengenezwa kwa kutumia mashine za kisasa zikiwemo robot kama ilivyo
kwenye viwanda vya magari katika nchi zilizoendelea. HAL ilianzishwa
mwaka 2007.
“Tuna kila kitu, mitaji kutoka taasisi za benki, intaneti yenye kasi,
mawasiliano ya simu, nguvu kazi ya kutosha na ardhi ya kutosha,
tunachohitaji ni watu kubadili mitazamo yao na kugeukia bidhaa zetu
nzuri,” alisema Hanspaul. Kenya, Uganda na Afrika Kusini wanatumia ‘War
Bus’ kupeleka watalii hifadhi za taifa na kuna taarifa zinazodai kuwa,
baadhi ya nchi zinayatumia magari kwenye shughuli za kijeshi.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment