Mahakama
Kuu Kanda ya Arusha imefanikiwa kusikiliza na kumaliza kwa zaidi ya
asilimia 90 ya mashauri yaliyofunguliwa katika kipindi cha mwezi Januari
hadi Agosti mwaka huu.
Kwa
mujibu wa takwimu zilizotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kanda
ya Arusha Mhe. Angelo Rumisha, jumla ya mashauri 737 kati ya 805
yaliyosajiliwa kuanzia mwezi Januari hadi Agosti 2017, yamemalizika.
Alisema
haya ni mafanikio ya kuridhisha kwa Mahakama Kuu kanda ya Arusha ambapo
kila Mhe. Jaji amesikiliza na kumaliza wastani wa mashauri 245. Hivi
sasa, Mahakama Kuu kanda ya Arusha ina jumla ya majaji watatu.
Katika
kuhakikisha inaondokana na mlundikano wa mashauri kwenye Mahakama
mbalimbali nchini, Mahakama ya Tanzania ilipanga idadi ya mashauri
yatakayosikilizwa na Majaji na Mahakimu. Kwa mujibu wa mpango huo, kila
Jaji anatakiwa kumaliza mashauri yasiyopungua 220 kwa mwaka na hakimu
Mashauri 250.
Akifafanua
takwimu za mashauri, Naibu Msajili alisema hadi kufikia Agosti 31,
mwaka huu, Mahakama hiyo imebakiwa na mashauri 809 ambapo kati ya
mashauri hayo, 788 yana umri wa kati ya miaka 1-2, mashauri 17 yana umri
kati ya miaka 3-5, mashauri 2 yana umri kati ya miaka 5-10 na mashauri
mengine 2 yana umri wa zaidi ya miaka 10.
Alisema
mashauri yote yenye miaka 10 na zaidi ni yale yaliyorudishwa kutoka
Mahakama ya Rufani baada ya kikao cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania kilichofanyika April mwaka huu.
Akizungumzia
Mahakama za Hakimu Mkazi na za Wilaya kwa Mikoa ya Arusha na Manyara,
Mhe. Rumisha alisema jumla ya mashauri 223 yana umri zaidi ya miezi 12,
kati ya mashauri hayo, ni mashauri mawili tu ndiyo ambayo Mahakama zina
mamlaka nayo ikiwa ni sawa na asilimia 1.3 ya mashauri yote yenye umri
zaidi ya miezi 12 hivyo mashauri mengi ya mlundikano ni yale ambayo
Mahakama hazina mamlaka nayo.
0 comments:
Post a Comment