RAIS John Magufuli ameagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi la Tanzania
(JWTZ) kwa kushirikiana na Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa
(Suma JKT), kuanza mara moja kujenga uzio kwenye eneo la kitalu A hadi D
lililopo eneo la Mererani, Simanjiro, ambalo kunapatikana madini ya
kipekee ya tanzanite.
Aidha, ameagiza kufungwa kwa kamera maalumu, kuweka uzio maalumu na
kutakuwa na eneo moja la mlango wa kutokea na kuingia ili kubaini wezi
wanaoiba madini hayo. Rais Magufuli alisema hayo jana eneo la Naisinyai
lililopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara wakati alipozindua barabara
ya lami yenye urefu wa kilometa 26 kutoka Kia/ Mererani, iliyojengwa kwa
gharama ya Sh bilioni 32.5 ambazo ni fedha zilizotolewa na Serikali ya
Tanzania.
Alisema sababu kubwa ya kuamua kujengwa kwa uzio huo na kufungwa
vifaa maalumu ni kudhibiti wizi wa madini hayo ya tanzanite, ambayo
yanapatikana nchini Tanzania pekee, lakini hayawanufaishi Watanzania
waliopo eneo hili wala serikali kupata mapato.Pia aliagiza vyombo vya
ulinzi na usalama, kuwaachia wawekezaji wanaoshikiliwa kutokana na suala
hilo la tanzanite na kushirikiana kwa pamoja na timu ya kupitia
mikataba ya madini iliyopo chini ya Profesa Palamagamba Kabudi ili
kuboresha mikataba ya madini na kila mmoja anufaike na madini hayo,
ikiwemo wananchi wanaozunguka maeneo ya migodiyote ya madini.
Alisema ni vyema sasa soko la tanzanite au mnada wa madini hayo,
kufanyika Simanjiro yanapochimbwa madini hayo na si mnada huo kufanyika
jijini Arusha. Alisisitiza kuwa lengo la soko hilo, kufanyika Simanjiro
ni kufungua fursa za biashara kwa wananchi, wachimbaji wadogo wa
tanzanite na madini mengine yanayotoka eneo hilo. Alisema eneo la
tanzanite lina ukubwa wa kilometa 81.99 za mraba, ambalo lipo Kitalu A
hadi Kitalu D na kilometa za mraba 13 zilizobaki ni namba moja hadi nne,
ambazo ni za wachimbaji wadogo.
Alisema tanzanite imeibwa sana na watu walifanya kama shamba la bibi
na kusisitiza kuwa viongozi wanapopewa mamlaka ya kusimamia rasilimali
za Taifa ni vyema wakazisimamia kwani Tanzania si nchi masikini, bali
umasikini unaletwa na watu wachache. “Katika uongozi wangu sitakubali
kuibiwa na nitasimamia mali za wananchi ziwe salama. Haiwezekani
unapopambana na jambo fulani yanaibuka mambo mengine ambayo yanataka
kukwamisha jambo unalolisimamia. Nasema hivi sitakubali kuona rasilimali
za nchi hii zinachukuliwa na wengine, hebu oneni mna madini haya,
lakini hamna hata gari la wagonjwa inasikitisha,” alieleza Dk Magufuli.
Alisema endapo tanzanite hiyo ingekuwa nchi nyingine, eneo la
Simanjiro lingekuwa kama Ulaya, lakini kwa mujibu wa ripoti iliyoundwa
na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, Job Ndugai, madini hayo
hayawanufaishi Watanzania wala wananchi wa eneo hili la Simanjiro.
Alisema asilimia tano tu ya madini ndiyo Tanzania inapata faida na
inayobaki yote ni faida kwa wawekezaji na wezi, lakini endapo
yangetumiwa vyema, kusingekuwa na matatizo ya kero ya barabara, gari la
wagonjwa, kero ya maji, na cha kushangaza kabisa wachimbaji wa madini
hayo hawana uhuru wa kununua au kuuza madini haya.
Akizungumza kuhusu uzinduzi wa barabara hiyo, Rais Magufuli
aliwapongeza wananchi wa Tanzania kwa kulipa kodi, zilizowezesha
wananchi wa eneo hilo la Simanjiro kupata barabara ya lami tangu kupata
uhuru. Alisema lengo la barabara hiyo kuwekwa lami ni kufungua milango
ya biashara pamoja na kupunguza kero ya usafiri waliokuwa wakiipata
wananchi hao. Alisema barabara hiyo itawezesha kuunganisha mawasiliano
baina ya mikoa mbalimbali nchini.
Baadhi ya wabunge waliofika kushuhudia uzinduzi huo, Mbunge wa Viti
Maalumu, Catherine Magige (CCM), James ole Millya ambaye ni Mbunge wa
Simanjiro (Chadema), walimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za
kuhakikisha anatatua changamoto mbalimbali za wananchi. Ole Millya
alisema wananchi wa jimbo lake, wanashukuru kwa ujio wa barabara hiyo
tangu nchi kupata Uhuru, lakini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa
gari la wagonjwa pamoja na kero ya maji, hivyo wanamuomba Rais Magufuli
kuwasaidia kuzitatua.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment