BAADHI ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Vijijini,
wamehoji ni kwa nini madiwani waliojiuzulu nafasi zao wilayani Arumeru,
wameajiriwa kwenye halmashauri hiyo, hali inayonyima fursa kwa wananchi
wengine wenye sifa na vigezo.
Diwani wa Kata ya Olturoto kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Baraka Simon alihoji kwa nini madiwani hao wafanye kazi
wakati walishajiuzulu.
“Ni kwa nini madiwani wa Wilaya ya Meru waliojiuzulu nafasi zao
wameajiriwa katika Halmashauri ya Arusha Vijijini na je, hamuoni kuwa
wanawanyima wenzao fursa za ajira, hii inashangaza,” alieleza Simon,
alipouliza swali la papo kwa papo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani
cha robo ya nne ya mwaka 2016/17 cha Halmashauri ya Wilaya ya Arusha
Vijijini.
Akijibu swali hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha
Vijijini, Dk Charles Mahera alisema ni kweli madiwani hao wapo katika
halmashauri hiyo, wanafanya kazi idara mbalimbali kwa kujitolea hadi
hapo serikali itakapotangaza nafasi za ajira mpya.
Alisisitiza kuwa waliomba nafasi za ajira katika idara mbalimbali,
hivyo wanasubiri ajira zitangazwe kisha wenye sifa waomba. Pia Diwani wa
Viti Maalumu, Lulu Ndosi (Chadema) alihoji ni kwa nini walimu wenye
digrii wanafundisha shule za msingi wakati wanastahili kufundisha shule
za sekondari.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment