Na Fatma Salum
MAELEZO
MWENYEKITI wa Kanisa la Good News
For All Ministry Askofu Dkt. Charles Gadi ametoa salamu za pole kwa wafiwa na
Watanzania wote walioguswa na msiba wa wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa
shule ya Msingi Lucky Vincent iliyotokea Karatu Mkoani Arusha wiki iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam, Askofu Gadi alisema kuwa kanisa lake linaungana
na familia za marehemu hao kuomboleza msiba huo mkubwa ulioacha pengo na
simanzi kwa familia na taifa kwa ujumla.
Askofu Gadi pia ameipongeza
Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kushirikiana bega kwa bega na familia
za wafiwa na wananchi wa Mkoa wa Arusha katika kuomboleza msiba huo jambo
ambalo limewaunganisha Watanzania na kuleta faraja kwa familia zilizopoteza
watoto wao.
“Tunaipongeza Serikali yetu ya
Mhe.Rais Dkt. John Magufuli kwa jinsi ilivyouchukulia msiba huu kwa uzito
mkubwa. Tumeguswa sana jinsi Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu alivyoshiriki
kwenye kuaga miili ya watoto hao.” Alisema Askofu Gadi.
Aidha Askofu Gadi alieleza kuwa
wanaunga mkono wito wa Serikali kwa madereva
wote nchini kuacha kuendesha gari
mwendo kasi na kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Katika hatua nyingine Askofu Gadi
amepongeza jitihada za Rais Magufuli kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo
ambayo ameizindua hivi karibuni ikiwemo ujenzi wa barabara za juu (fly overs),
reli mpya ya kisasa (standard gauge) na miradi mingine.
“Tunaamini kwa kasi hii, Rais Magufuli
na Serikali yake watailetea nchi yetu maendeleo makubwa ya kupigiwa mfano hivyo
nawaomba Watanzania wenzangu tuendelee kumuombea na tufanye kazi kwa bidii kwa
ajili ya maendeleo ya taifa letu.” Aliongeza Askofu Gadi.
Katika mkutano huo na waandishi
wa habari, Askofu Gadi aliongoza maombi ya kumuomba Mungu mvua iache kunyesha
mkoani Dar es Salaam na ukanda wa pwani badala yake Mungu aielekeze kwenye
mikoa mingine ambako inahitajika kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine.

0 comments:
Post a Comment