Picha ya pamoja
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KIKOA CHA JPC KATI YA TANZANIA NA UGANDA CHAFUNGULIWA JIJINI ARUSHA
Tanzania na Uganda zimetakiwa kushirikiana kwa pamoja kutumia rasilimali walizonazo kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa pande zote mbili.
Kauli hiyo imetolewa leo kwa pamoja jijini Arusha na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya walipokuwa wanafungua Kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya nchi hizo mbili.
Walieleza kuwa kikao hicho ni cha kwanza kufanyika tokea makubaliano yaliposainiwa mwaka 2007 na kinafanyika kufuatia maelekezo ya Marais wa nchi hizo waliyoyatoa wakati wa ziara ya Rais Yoweri Museveni nchini mwezi Februari 2017.
"Kikao hiki ni fursa kwa wataalamu wetu kujadili na kubuni mfumo bora na endelevu wa Ushirikiano utakaoleta tija kwa pande zote mbili katika kila eneo iwe miuondombinu, biashara, viwanda, uwekezaji, usafiri wa anga na majini, kilimo, elimu, afya, mazingira, utalii, nishati na ufugaji.
Balozi Mwinyi alieleza kuwa licha ya nchi hizo mbili kuwa na mahusiano mazuri tokea miaka ya 60 lakini kiwango cha biashara kati yao ni kidogo mno hivyo aliwashauri wajumbe wa JPC kubuni mikakati itakayonyanyua kiwango cha biashara.
Kwa upande wake, Balozi Mugoya aliwambia wajumbe wa kikao hicho kuwa Tanzania na Uganda sio tu ni nchi majirani, bali ni nchi zenye urafiki mkubwa, hivyo alihimiza urafiki huo utumike kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa pande zote. " Tuna changamoto za ukame, uhaba wa maji na malisho kwa wafugaji na wakulima wanaoishi katika mipaka yetu. Hivyo alisisitiza umuhimu wa kikao hicho kutoa mapendekezo ya namna ya kushirikiana kwa kutumia rasilimali zilizopo mipakani na nyinginezo kukabiliana nazo".
Kikao hicho cha JPC kitafungwa rasmi siku ya Jumatano na Mawaziri wa Mambo ya Nje ambapo kabla ya kufungwa kutashuhudiwa uwekaji saini wa makubaliano mbalimbali kati ya Tanzania na Uganda. Makubaliano hayo ni pamoja na Ushirikiano katika kuboresha bandari, usafiri wa majini na huduma ya usafiri wa reli; kuendeleza mradi wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo; Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na lile la Uganda katika masuala ya usalama, Ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi naTeknolojia na Wizara ya Elimu ya Uganda, Ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji la Tanzania na la Uganda na Ushirikiano katika huduma za usafiri wa Anga.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, 03Aprili, 2017
|
0 comments:
Post a Comment