Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Wanafunzi
wa shule za Msingi mkoani hapa wametakiwa kuwa makini na kutokuwa na
tamaa ya kuomba “lift” au kupewa chipsi au kushawishiwa kwa namna yoyote
ile na watu ambao hawafahamiana nao pindi wanapokwenda shule au
wanaporudi majumbani kwao.
Hayo
yalielezwa na Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa
Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu wakati alipokuwa akitoa elimu ya
Ukatili na Unyanyasaji wa kijinsia katika vipengele vya ubakaji,
ulawiti na vipigo kwa wanafunzi 63 wa Elimu Maalum kitengo cha viziwi
katika shule ya Msingi Meru iliyopo halmashauri ya jiji la Arusha.
Alisema
baadhi ya wanafunzi wanajikuta wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa
kijinsia kama ubakaji na ulawiti baada ya ushawishi mdogo mdogo kwa
kupewa lift, kununuliwa vyakula mbalimbali kama vile chipsi na
kadhalika.
“Baadhi
ya vitu ambavyo vinasababisha ushawishi na hatimaye wanafunzi
wanafanyiwa ukatili wa kubakwa au kulawitiwa bila hata wao wenyewe
kudhani kama hali hiyo inaweza kutokea ni pamoja na lift za magari au
pikipiki, kununuliwa vyakula mbalimbali kama vile chipsi.”. Alisema Mkuu
huyo wa Dawati Happyness Temu.
“Sio watu wote wana nia mbaya katika utoaji wa “lift” ila kuna wachache si wema na hawawezi kujulikana yupi
mwema na yupi mbaya hivyo wazazi wanatakiwa wawafuatilie kwa ukaribu na
kuwaeleza uhalisia wa mabadiliko ya maisha watoto wao ili kuwaepusha na
watu wenye nia mbaya dhidi yao”. Aliongeza Mkaguzi huyo wa Polisi
Happyness Temu.
Wakiongea
kwa lugha ya ishara na kutafsiriwa na walimu wa shule hiyo Veila Wilson
na John Maukiri, baadhi ya wanafunzi walionyesha kufurahia elimu hiyo
na kupata ufahamu juu ya hatua wanazoweza kuchukua katika kujiepusha na
vitendo vya ukatili na unyanyasaji na pia walifahamu hatua za kuchukua
mara watakapofanyiwa ukatili wa aina yoyote.
Baadhi
ya wanafunzi hao walikiri kufanyiwa hasa ukatili wa vipigo majumbani
mwao huku mkuu huyo wa Dawati kuahidi kuwasilikiza walalamikaji na
kufuatilia kwa ukaribu kwa nia ya kukomesha tabia hiyo.
Naye
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambayo inamchanganyiko wa wanafunzi wa elimu
ya kawaida na elimu maalum Bw.Musa Luambano, alilishukuru Jeshi la
Polisi kupitia kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto kwa kutoa elimu
hiyo kwa wanafunzi hao ambayo itawasaidia kujua hatua za kuchukua pindi
wanapofanyiwa ukatili lakini pia wao watakuwa mabalozi kwa wengine
katika kuwaelimisha.
Alisema
kitendo cha Jeshi la Polisi kufika katika shule hiyo na kutoa elimu kwa
wanafunzi wa kitengo cha elimu maalum ni ishara ya hatua nzuri katika
kuongeza ushirikiano kati ya Jeshi hilo na wanafunzi wa aina hiyo na
kutoa wito kwa ofisi mbalimbali kupeleka watumishi wao ili waweze
kujifunza elimu ya lugha ishara ambayo itaweza kuwasaidia katika
kuhudumia makundi yenye uhitaji maalum kama vile viziwi.
0 comments:
Post a Comment