Arusha
Home » » CCM YAPATA USHINDI WA KIMBUNGA SIMANJIRO

CCM YAPATA USHINDI WA KIMBUNGA SIMANJIRO

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Simanjiro mkoani Manyara, kimepata viongozi 223 kati ya 281 wa vitongoji na wengine 48 kati ya 55 wa vijiji waliopita bila kupingwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, unaotarajia kufanyika Jumapili.
Katibu wa UVCCM Wilaya ya Simanjiro, Bakari Mwacha alithibitisha hayo jana wakati Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Brown ole Suya akizindua kampeni ya CCM ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwenye mji mdogo wa Mirerani.
Mwacha alisema hadi sasa kabla ya uchaguzi huo, CCM imepata ushindi wa asilimia 87 kwenye uchaguzi wa ngazi ya vijiji na asilimia 88 katika vitongoji vya wilaya hiyo, baada ya wagombea wao kupita bila kupingwa.
Katibu Uchumi na Fedha wa CCM mkoani Manyara, Lucas Zacharia aliitaka Chadema kutoeneza maneno ya chuki, fitina na uongo kuwa yeye alitoa rushwa ili wagombea wao waondolewe ilhali walikosea kujaza fomu zao.
Zacharia ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Endiamtu, alisema wagombea wa Chadema walikosea kwa kuandika majina yao, hivyo wajilaumu wao wenyewe na siyo kuchafua majina ya watu kuwa rushwa ilitumika ili waondolewe.
“Kama ni uchawi watafutane wao wenyewe na kama ni uzembe walifanya wao wenyewe na siyo kudanganya wananchi kuwa eti nilitoa rushwa kwa wasimamizi wa uchaguzi huo ili CCM tupite bila kupingwa,” alisema Zacharia.
Alisema kwenye vitongoji vyote 12 vya Kata yake ya Endiamtu, wagombea wote wa CCM walipita bila kupingwa, baada ya wagombea wa Chadema kukosea kujaza fomu na kujidhamini wao wenyewe badala ya chama chao.
Chanzo;Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa