MBUNGE wa Arusha Godbless Lema (CHADEMA), amemtaka Mkuu wa Mkoa mpya, Mhandisi Everist Ndikilo, kuhakikisha anaepuka kuwa chanzo cha mivurugano kama ilivyokuwa kwa jiji la Mwanza analotoka.
Rais Jakaya Kikwete, juzi alifanya uteuzi wa wakuu wa mikoa wapya wanne, kuwahamisha wengine sita na wengine watapangiwa kazi nyingine.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Lema alisema kuwa ni vema Ndikilo akajiepusha kulitumia jeshi la polisi katika kukandamiza demokrasia.
Lema, alisema kuwa iwapo Ndikilo ataheshimu na kuweka demokrasia mbele na kuepuka kuingilia masuala ya halmashauri, watakuwa tayari kushirikiana naye.
“Ndikilo ni kati ya wakuu wa mikoa waliotumika kuivuruga ngome ya CHADEMA huko Mwanza …sasa kama atakuja katika jiji hili na yale aliyoyafanya Mwanza, hasifikiri eneo hili litakuwa jepesi kwa utawala wake,” alisema.
Alisema kuwa Jiji hilo lina watu makini ambao hawapo tayari kuona demokrasia ikikandamizwa.
Mbunge huyo, alisema kuwa usuluhishi wa masuala mbalimbali ndiyo jambo la msingi litakalomsaidia aongoze vyema.
Aidha, Lema alisema kuwa ni vema pia Magesa Mulongo ahakikishe anatumia vyema utendaji kazi alioupata katika Jiji la Arusha ili kuweza kumudu na kufanikisha kuongoza vyema Jiji la Mwanza.
“Azingatie muongozo alioupata hapa mwishoni na kama ataenda kufanya kazi kwa kutumia dola, nina hakika ngome hiyo itamshinda na itakuwa wakati wake mgumu katika utawala wake,” alisema.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment