Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JIJI la Arusha limekumbwa na taharuki baada ya kuibuka kwa matukio
ya wanawake wanaoendesha magari kuvamiwa na kupigwa risasi na watu
wasiofahamika ambao hutoweka bila kuchukua chochote.
Hadi sasa, wanawake watatu wamekumbwa na kadhia hiyo huku mmoja akifariki.
Aidha, Jeshi la Polisi linaangalia uwezekano wa kufunga kamera ili
kukabiliana na matukio ya uhalifu yanayolikumba Jiji, na kwa sasa
wanaendelea na majadiliano na wadau mbalimbali ili kufanikisha hilo.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, jana alithibitisha
kutokea kwa matukio hayo, aliyosema kuwa mawili yametokea eneo la Sakina
kwa Iddi na moja Mbauda, ingawa hakuwa tayari kutaja jina la mwanamke
huyo aliyedai kuwa alipigwa risasi lakini haikumpata.
Alisema hadi sasa hawajajua sababu ya matukio hayo, ambayo walengwa
wakuu wamekuwa ni wanawake wanaoendesha magari, hivyo akaomba jamii
kutoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa wahalifu hao.
Sabas, alimtaja aliyefariki kuwa ni Shamim Yulu, (30),
ambaye alipigwa risasi shingoni juzi majira ya saa 3.30 usiku wakati
akikaribia kufika kwenye lango la nyumba yake maeneo ya Sakina kwa Iddi
wakati akiendesha gari yake yenye namba za usajili T 566 BYA aina ya
Toyota Ipsun.
“Akiwa peke yake, alipokaribia geti la nyumbani kwake ghafla aliona
pikipiki ambayo namba zake za usajili zilikuwa zimetolewa ikiwa na
vijana wawili, ambao walimsimamisha na kufyatua risasi moja hewani…
“Kitendo kilichomfanya marehemu kuongeza kasi ya gari lakini
majambazi hao walifanikiwa kumjeruhi na kumpora simu mbili aina ya nokia
na Samsung,” alisema Sabas na kuongeza marehemu alifariki dunia wakati
akipatiwa matibabu kwenye hospitali ya Selian.
Kamanda Sabas, alisema tukio lingine lilitokea mwanzoni mwa wiki
eneo hilo hilo la kwa Iddi, ambako majira ya saa 1:00 usiku, Florah
Porokwa alipigwa risasi kifuani wakati akiendesha gari lake aina ya
Toyota Harrier.
Alisema wakati mwanamke huyo akielekea nyumbani kwake, alivamiwa na
watu wawili waliyokuwa kwenye bodaboda na kumpiga risasi lakini
alijitahidi kuendesha gari hilo mpaka karibu na nyumbani kwake, ambako
alipoteza fahamu kutokana na kutokwa na damu nyingi kabla ya majirani
kumsaidia kumwahisha hospitali.
Mume wa Florah, Edward Porokwa ambaye ni mkurugenzi wa Shirika liliso
la kiserikali la kutetea haki za wafugaji, (Pingo’s), aliiambia
Tanzania Daima jana kuwa, mke wake anaendelea vizuri ingawa bado
amelazwa kwenye hospitali ya Selian.
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi linawashikilia watu wanne
kuhusiana na matukio ya kigaidi, ambako mmoja kati yao, Adam Pakasi,
(34), amekutwa na bunduki ya kutengeneza kienyeji, risasi 38 za short
gun, ganda moja la risasi lililotumika pamoja na mafuta ya kusafishia
bunduki yaliyokuwa yamewekwa kwenye chupa ya maji ya kunywa.
Kamanda Sabas, ambaye hakuwa tayari kutaja majina ya watu wengine
watatu wanaowashikilia kwa madai kuwa bado wanaendelea kuwahoji, alisema
walifanikiwa kuvipata vitu hivyo baada ya kupekuwa nyumbani kwa Pakasi
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment