Home » » ASIMULIWA ALIVYOPIGWA BOMU ARUSHA,AKAZIMIA SIKU 14

ASIMULIWA ALIVYOPIGWA BOMU ARUSHA,AKAZIMIA SIKU 14

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti wa wa Chadema, Freeman Mbowe
 
“Nilizinduka siku ya pili wakati kumekucha, nikauliza watu walionizunguka, nipo wapi?Nilikuwa nashangaa nimelala kitandani katika mazingira tofauti nikiwa na maumivu makali mwilini. Sikukumbuka nilikuwa wapi.
“Kumbe nilikuwa nimefanyiwa upasuaji sehemu mbalimbali za mwili wangu,” anakumbuka, Gabriel Lucas, (50), baba wa watoto wanne na mkazi wa Lemara, jijini Arusha.
Anasema anakumbuka kitendo cha mwisho alichofanya ni kusimama na kujinyoosha wakati akiwa kwenye mkutano wa Chadema wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani wa kata nne za jijini Arusha.
Katika uchaguzi huo, Chadema ilishinda kata zote za Themi, Elerai, Kimandolu na Kaloleni na kuvibwaga vyama vya CCM na CUF.
Anasema akiwa amekaa kusikiliza mkutano huo uliokuwa ukihutubiwa na Mwenyekiti wa wa Chadema, Freeman Mbowe, na kutokana na yeye kuwa mmoja wa walioandaa mikutano ya kampeni, alijihisi kuwa amechoka.

Anasema kwa kawaida chama chao huwa kinafanya harambee kuchangisha fedha kwa ajili ya maendeleo yao na kutokana na utaratibu huo, Mbowe na wenzake waliteremka jukwaani na kuanza kuchangisha fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya chama.

Lakini kabla ya shughuli hiyo kuanza, “nikiwa nimekaa kwa muda kwenye kiti, nilijikuta nikisimama kujinyoosha na wakati nikifanya hivyo, niliona kwa mbali kidogo gari aina ya Landrover pick up na nyuma yake kulikuwa na gari aina ya Noah ambayo madirisha yake yalibandikwa karatasi nyeusi za nailoni.

“Kutoka kwenye gari hilo nilimwona mtu mmoja akirusha mfuko wa malboro eneo ambako watu wapo na kitu hicho kilitua kama mita mbili hivi toka sehemu nilipokaa.

“Sasa mimi kwa kuchoka, manake toka asubuhi nilikuwa mwandaaji wa huo mkutano, nilinyanyuka kwenye kiti kwa lengo la kujinyoosha, na kabla kitu hicho hakijatua chini, na hiyo ilikuwa ni kitendo cha haraka, mrushaji aliteremka kwenye hiyo Cruiser na kuingia gari ya Noah na kutokomea.

“Ghafla nilisikia mlipuko mkubwa baada ya kitu hicho kutua chini. Sikuweza kujijua tena, kumbe nilikuwa nimeanguka chini, sijijui, niliumia vibaya kwa vipande vya chuma. Naambiwa mama mmoja alikuwa amekaa jirani yangu (ni kiongozi wa chama, alikuwa Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema, (Bawacha), Kata ya Sokoni One, Judith Moshi, huyu alikuja kufa papo hapo.Walikuwepo watoto wawili wasichana jirani yetu, nao walipoteza maisha hapo hapo.

“Nikiwa na fahamu kidogo, nilijikuta nikiwa na wengine kwenye gari huku damu ikiwa imetapakaa, tulifikishwa kwanza Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, hapo walikataa kutupokea na wakakimbia wote, sijui ni kwa nini, lakini tukapelekwa Hospitali ya Rufaa ya Selian ambako walitupokea,” anakumbuka na kuongeza:

“Hapo Mount Meru hospitali tulikuwa tumelazwa chini sehemu ya mapokezi huku damu ikiwa imetapakaa sijiwezi nakawaulizaa, ‘mnatuacha tunakufa kweli?.

Anasema baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Selian, inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, hakujitambua tena hadi asubuhi siku ya pili yake.

“Tangu wakati huo sikujitambua hadi kesho yake asubuhi nilipozinduka kidogo, sikuweza kujua nani walitupeleka hospitali.

“Nikaja kuzinduka karibu kumekucha Jumapili, nimeshafanyiwa upasuaji wa kutoa vipande vya vyuma mwilini.Sikuwa na nguvu hata ya kuongea.

Anakumbuka siku hiyo, Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal, na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, walienda kumuona kwa nyakati tofauti.
Anamkumbuka pia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, kuwa alienda hospitalini hapo kumuona naye anakumbuka aliuzwa, ‘unafikiria hii hali imetokeaje?’

“Nakumbuka nilimjibu, ‘wewe ni mlinzi  wa amani mkoani hapa, unao polisi na vyombo vingine usalama, lakini umeamuru watupige halafu unaniuliza hali hii imetokeaje,” anasema.

Anasema alikuwa akizungumza hivyo huku akilia kwa maumivu makali sana.“Najua Mkuu wa Mkoa alijisikia vibaya kwa kumjibu vile kwa sababu watu walikuwepo na waandishi wa habari pia. Nilijisikia vibaya. Hapo hapo nilipoteza fahamu kwa sababu nilikuwa bado navuja damu na nikapelekwa chumba cha uangalizi maalum (ICU).

Anasema alikaa ICU kwa siku zaidi ya 14 na akazinduka na kupelekwa wodini ambako alikaa kwa muda wa zaidi ya siku 40 hivi na baadaye aliruhusiwa lakini akawa akiendelea kupata matibabu kutoka nyumbani.

Anasema mpaka sasa anaendelea kupata matibabu hospitalini hapo na anasumbuliwa sana na miguu na njia ya mkojo.Akizungumzia tukio lile, Gabriel, ambaye kwa sasa ni mratibu wa masuala ya siasa, Ofisi ya Mbunge wa Arusha Mjini, anasema kwanza anamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kumnusuru katika tukio lile na kumjalia uhai hadi sasa.

“Wenzangu walifariki pale pale, mama mmoja na watoto wawili. Wapo pia waliopoteza viungo, wengi tu. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu, pamoja na majeraha makubwa na maumivu makali bado nipo salama,” anasema.

Pia anasema anakishukuru Chadema, chama ambacho kimetumia zaidi ya Sh. Milioni 14 kwa matibabu yake, achia mbali fedha ambazo imetumia kuwatibu majeruhi wengine ndani na nje ya nchi.

Anasema Chadema kilifanya hivyo bila ya ubaguzi wo wote.Anakishukuru pia chama hicho kwa kutekeleza kwa vitendo kauli za viongozi wao wanazihubiri majukwaani, lakini mwisho anasema, “sitaacha kuilaani CCM na Serikali yake.
Anasema chama hicho (CCM) hakijawahi kuwa tegemeo la Watanzania tangu zamani na mbaya zaidi sasa kimekuwa sababu ya Watanzania kuteseka na kupoteza maisha yao.

Anawasihi Watanzania wasimamie haki yao na kuhakikisha dhuluma isiendelee kutawala, na anawalaani polisi kwa maelezo kuwa badala ya kufanya kazi yao ya usalama wa raia sasa wamekuwa adui wa raia.

“Watanzania tumekuwa tukipigwa na serikali, na hivyo tumekuwa kama tuliong’atwa na mbwa koko mwenye kichaa na hatuna wa kumlalamikia,” anasema na kuhoji, CCM walidai kuwa sisi tumejilipua wenyewe, sasa haya mabomu yanayoendelea nao wamejilipua wenyewe?”
Anadai serikali imeshindwa kuwatetea na sababu ya msingi ya kutofanya hivyo wanaijua wao wenyewe.

Tangu kutokea kwa mlipuko wa bomu hilo, Chadema kimekuwa kikishinikiza serikali kuunda tume huru ya uchunguzi lakini serikali kwa upande wake imekataa kuundwa kwa tume hiyo.

Kumekuwa na madai tofauti kati ya pande mbili, serikali ya CCM na Chadema, huku CCM awali ikinukuliwa na makada wake wakidai kuwa Chadema ndiyo waliojilipua na kwa upande mwingine Chadema inadai kuwa Serikali ya CCM kwa kutumia polisi ndiyo iliyowalipua kwa mabomu.

Kutokana na hali hiyo, Chadema imeomba Rais Jakaya Kikwete kuunda tume huru ya uchunguzi wa sakata hilo, jambo ambalo limepingwa.

Baadhi ya watu wanasema kama tume hiyo ingeundwa, huenda ingeweza kutoa ufumbuzi wa matukio ya mabomu yanayoendelea kutokea jijini hapa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa