Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MAWAKILI wa utetezi kwenye shauri la utakatishaji fedha
linalowakabili washitakiwa wanne akiwemo wakili maarufu, jijini hapa,
Median Mwale, wameibua hoja juu ya uhalali wa kutumika kwa sheria ya
kuzuia utakatishaji fedha.
Hoja hiyo nzito kisheria inaeleza kwamba sheria hiyo haifai kutumika
kwa sababu haijatangazwa kwenye gazeti la serikali baada ya kusainiwa
na rais.
Mbali ya Mwale, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Elius Ndenjembi, Don Bosco Gichana na Bonifasi Mimbwa.
Waliwalalamikia wateja wao kufunguliwa mashitaka kwa kutumia sheria
zilizoidhinishwa kuanza kutumika baada ya wao kukamatwa jambo walilodai
ni kinyume cha sheria.
Mawakili hao pia wamelalamikia ucheleweshwaji wa makusudi wa kuanza
kusikilizwa kwa shauri hilo unaofanywa na upande wa serikali kwa kigezo
cha upelelezi haujakamilika, huku wateja wao wakiendelea kuteseka
rumande kwa miaka mitatu sasa.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na wakili wa utetezi, Omary Iddi Omary, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Devota Kamuzora.
Wakili huyo anashirikiana na mawakili Mosses Mahuna na Modest Akida,
huku upande wa serikali ukiwakilishwa na wakili, Tumaini Kweka.
Waliiomba mahakama hiyo iridhie ombi lao la kupeleka mkanganyiko huo
wa kisheria Mahakama Kuu ili ukapatiwe tafsiri ya kisheria ikiwemo
uhalali wa sheria hiyo waliyodai kuwa mchakato wake una upungufu kwa
kuwa haujatangazwa kwenye gazeti la serikali baada ya rais kuisaini ili
ianze kutumika.
“Sheria hiyo iliwekwa kwenye gazeti la serikali Januari 12, 2006
kabla ya kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete Januari 15, 2007 ukiangalia
tarehe hizo mbili utaona ilitangazwa kabla rais hajaisaini kuiridhia na
baada ya kusainiwa haijatangazwa ili ianze kutumika hivyo sheria hii
haiwezi kuwa halali kutumika hadi itakapotangazwa.
“Mheshimiwa hakimu, kutokana na ukiukwaji wa taratibu hizo, unafanya
sheria ya uzuiaji utakasaji wa fedha haramu ya mwaka 2006 isiwepo, hii
ina maana hata washtakiwa hawa wanashikiliwa kwa kutumia sheria ambayo
haipo.
“Hata kosa wanaloshitakiwa nalo halipo kwenye sheria za sasa, katika
mazingira hayo hakuna shaka kuwa hapa hakuna mashtaka sahihi,” alisema
wakili Omary.
Wakili huyo aliieleza mahakama kwamba wateja wake wameshitakiwa kwa
kosa la kula njama kutenda kosa kinyume cha sheria huku kwenye maelezo
ya kosa ikitumiwa sheria nyingine ambapo wanadaiwa kukiuka sheria ya
uzuaji utakasaji fedha ya mwaka 2006 jambo alilodai kuwa linakiuka
sheria ya uendeshaji mashauri ya jinai (CPA).
Akijibu hoja hizo wakili wa serikali, Kweka alidai hazina msingi kwa
kuwa sheria hutumika baada ya kupitishwa na Bunge na kuwa imefuata
michakato yote ndipo huanza kutumika.
“Nafikiri wameleta malalamiko kwenye eneo lisilo sahihi, kwani hata
kwa mujibu wa uanzishwaji wa mahakama hii sidhani kama wewe (hakimu)
unaweza kuamua mashauri ya Manyara, hii ni sawa na kumtuma mtoto
akachukue chakula cha mlinzi,” alisema wakili Kweka jambo lilomfanya
hakimu kuingilia kati na kumtaka afute kauli yake ya kumfananisha yeye
na mlinzi.
Baada ya malumbano ya kisheria, hakimu Kamuzora aliahirisha shauri
hilo hadi Mei 12, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi mdogo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment