Arusha
Home » » POLISI WATANGAZA BINGO WALIPUAJI NIGHT PARK

POLISI WATANGAZA BINGO WALIPUAJI NIGHT PARK

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI),Isaya Mngulu
Jeshi la Polisi nchini limetangaza zawadi ya Sh. milioni 10 kwa atakayewezesha kukamatwa kwa  watu waliotumia mabomu kulipua  baa ya Night Park mwishoni mwa wiki iliyopita.
 Katika mlipuko huo, watu 17 wameripotiwa kujeruhiwa kati ya hao, waliobaki wodini kuendelea na matibabu ni nane baada ya wengine kuruhusiwa.

Wanaondelea na matibabu ni  Evance Maleko, Evarist Richard, Petro James, Christian Zakaria, Pius Shayo, Antelus Ishengoma, Sudi Ramadhani na Mariam Hansi aliyeko hospitali ya Selian.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Isaya Mngulu, alisema uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo umebaini kuwa bomu lililolipuliwa Aprili 13, mwaka huu, saa 1:30 asubuhi kwenye baa hiyo, ni la kutengenezwa kienyeji.

Mngulu alisema wataalamu wa mabomu waligundua bomu lingine lililokuwa kwenye mkoba ulioegeshwa kwenye kiti katika baa ya Washington,  pembeni mwa baa hiyo.

“Bomu hili tumeligundua baada ya tukio hili kutokea na saa sita usiku tukaligundua, lakini halijalipuka na tunalo kwa ajili ya kuchunguza tujue limetengenezwa kwa kutumia vifaa gani,” alisema.

Alisema hata  bomu hilo ni la kutengenezwa kienyeji, jambo lililowafanya waelewe hata hilo lililolipuka ni la kienyeji.

Mngulu alisema kutokana na kukithiri kwa matukio hayo nchini kwa sasa, ni vema wananchi na hasa wale ambao wapo maeneo ya mkusanyiko, wakachukua tahadhari za uhakika, kwani siyo vema kumwamini hata rafiki yako.

“Ni vizuri ukajiridhisha alichobeba rafiki yako kwenye mkoba na ukitilia wasiwasi bora utoe taarifa polisi na siyo kukaa kimya hadi madhara yakatokea,” alisema.

Alitoa rai kwa wamiliki wa kumbi za starehe, makanisani, misikitini na maeneo ya mikusanyiko kujitahidi kuweka kifaa cha CCTV ili kuwezesha kubaini wahalifu pale uuhalifu unapotokea.

Alisema hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwa kuwa wana kifaa cha CCTV kilichofungwa Night Park, wana hakika muhusika atapatikana.

Alisema matukio ya milipuko ni mengi kutokea nchini kwa sasa na yanatokea maeneo mbalimbali na siyo Arusha peke yake, isipokuwa wote wanaokamatwa na milipuko hiyo kama Dar es Salaam na Tanga ni vijana wadogo ambao hawajawahi hata kupita jeshini.

Kuhusu Sikukuu za Pasaka, alisema kila mkoa umepewa maelekezo kwa Kamanda wa Polisi kutumia mbinu zao zote na vifaa walivyonavyo kama farasi na mbwa ili kulinda usalama wa ibada za sikukuu hizo.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa