MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, ameupongeza
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kutoa bure huduma za upimaji
wa afya kwa wananchi.
Pongezi hizo alizitoa hivi karibuni baada ya kupata maelezo ya
utendaji wa mfuko huo kutoka kwa Meneja wa NHIF Arusha, Anicia
Ng’weshemi, wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Maendeleo
Tengeru.
“Kazi mnayoifanya ni nzuri kwani matatizo kama sukari, shinikizo la
damu na uzito uliozidi yamekuwa tishio, hivyo mmefanya kazi nzuri…
hongereni sana,” alisema Balozi Iddi aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa
kufunga maonyesho hayo.
Katika maonyesho hayo zaidi ya watu 600 walipata huduma za kupima
magonjwa yasiyoambukizwa sambamba na elimu ya kujikinga nayo.
NHIF imetoa huduma za kupima afya kwenye maeneo mbalimbali ya nchi
kwa lengo la kuwasaidia wananchi kufahamu afya zao na kuwapa ushauri wa
kitaalamu.
Mbali na huduma za upimaji, NHIF pia ilikuwa na dawati la elimu kwa
umma ambalo kazi yake ilikuwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kujiunga na
mfuko huo, Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na Tiba kwa Kadi (TIKA).
Wakizungumza katika banda la mfuko huo, wanachama na wananchi wengine
waliofika kwa lengo la kupata huduma walieleza kufurahia huduma hizo
na kusema ni mkombozi kwa wananchi hasa kipindi hiki ambacho gharama za
matibabu ni kubwa.
Akitoa ushauri kwa wananchi, Ofisa Udhibiti Ubora wa NHIF, Dk. Peter
Nyakubega, alisema ni vema wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya
zao mara kwa mara, hali itakayowasaidia kujitambua
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment