Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Katika kile
kinachooneka kuzidi kuhamasisha na kuimarisha Ulinzi na Usalama maeneo
mbalimbali ya Mkoa huu, Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Polisi Jamii mkoani
hapa limetoa vizibao 15 kwa kikundi cha Ulinzi Shirikishi cha Muklati kilichopo
Ngaramtoni wilayani Arumeru.
Akizungumza wakati
wa makabidhiano wa vizibao hivyo leo tarehe 08.01.2014 Adhuhuri, Mkuu wa
Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP)
Mary Lugola alisema kwamba, Jeshi hilo limeonyesha njia ili kuweza
kuwahamasisha wananchi wa maeneo mbalimbali mkoani hapa waweze kuunga mkono
juhudi hizo hivyo kujitolea kwa ajili ya kusaidia vikundi hivyo.
Alisema kikundi
hicho kilichopo Ngaramtoni kimeweza kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama na hali
hiyo inatokana na uzalendo walionao vijana hao. Alisema elimu ya ulinzi
waliyopata vijana hao imewawezesha kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu hali
ambayo imesaidia kupunguza vitendo vya uhalifu na kufanikiwa kukamata silaha
mbalimbali zilizotengenezwa kienyeji.
Mkuu huyo wa Polisi
Jamii aliendelea kusema kwamba, vizibao hivyo vyenye maandishi ya “ULINZI
SHIRIKISHI MKOA WA ARUSHA” vitawasaidia kwenye utendaji wao wa kazi hasa katika
suala la utambulisho. Alisema ni vigumu kumtambua mtu au kutambuana mara moja
lakini kupitia vizibao hivyo wananchi wa eneo hilo watawatambua kiurahisi na
wao kutambuana.
Naye Polisi Tarafa
wa eneo hilo ambaye pia Mkuu wa kituo cha Polisi Ngaramtoni, Mkaguzi Msaidizi
wa Polisi Elibariki Kileo alizidi kuwasisitiza wananchi wa Tarafa hiyo
wajitokeze katika kusaidia kikundi hicho na vingine vilivyopo katika mitaa na
vitongoji mbalimbali vya Tarafa hiyo kwani usalama uliopo katika eneo hilo ni
matunda ya kikundi hicho.
Aidha kwa upande wake
Mwenyekiti wa mtaa wa Muklati Bw. Naima Saitabao alisema kwamba toka kikundi
hicho kianzishwe mwaka 2007 hali ya uhalifu imezidi kupungua ikilinganishwa na
kipindi cha nyuma. Alisema ushirikiano uliopo kati ya Polisi Tarafa wa eneo
hilo, uongozi wake pamoja na wananchi uliwezesha kuanzisha kikundi hicho ambapo
kimeweza kudhibiti matukio mengi ya uhalifu kwa kushirikiana na Jeshi la
Polisi.
0 comments:
Post a Comment