Arusha
Home » » Padri ampongeza Kagasheki kuachia ngazi

Padri ampongeza Kagasheki kuachia ngazi

PADRI Pius Shao wa Parokia ya Indumeit ya Kanisa la Katoliki Jimbo la Arusha, iliyoko katika Kijiji cha Kamwanga, amempongeza aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki, kwa kukubali kujiuzulu baada ya kushutumiwa kuhusika na uzembe wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili. Padri Shao alisema hayo hivi karibuni, wakati akiendesha ibada kanisani hapo, ambapo alisema Balozi Kagasheki alionyesha ukomavu wa kisiasa.

“Ni viongozi wachache Tanzania ya sasa wanaoweza kuwa na moyo wa kizalendo namna hii, Balozi Kagasheki alifanya kitendo cha kiungwana na kizalendo, hii inadhihirishia umma kwamba ana uchungu na taifa lake,” alisema Padri Shao.


Katika hatu nyingine, aliwataka wazazi na walezi wilayani Longido kuwalea watoto katika maadili mema ya kiimani pamoja na kuwajengea misingi imara ya elimu kwa ajili ya siku zijazo.

“Wazazi wengi wamekuwa chanzo cha watoto wengi kuharibika kimaisha, wamejisahau katika malezi na hali hii imesababisha kuwapo kwa kundi la vijana lisilo na maadili ambalo ndiko kunakopatikana vibaka, wezi na walevi wa kupindukia, matumizi ya madawa ya kulevya, mimba za utotoni na hata maambukizi ya ugonjwa wa hatari wa Ukimwi,” alisema Padri Shao na kuongeza:

“Nawaomba viongozi wa dini, serikali pamoja na jamii kwa ujumla kuhakikisha mnashirikiana kuwalea watoto hawa katika msingi bora na kuzilinda ndoa zetu kwani ndoa zikiwa imara ndiyo kunakupatikana malezi bora ya watoto wetu,” alisema.

Katika utekelezaji Operesheni Tokomeza Ujangili, madudu mengi yaliyojitokeza yaliibuliwa na ripoti ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira ya Bunge na kusababisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David Mathayo na Balozi Kagasheki kujiuzulu.

Chanzo:Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa