Arusha. Mtandao wa Mashirika ya Wafugaji
(Pingos Forums) umependekeza kufikishwa mahakamani kwa mawaziri wanne
ambao uteuzi wao umetenguliwa na Rais Jakaya Kikwete kutokana na kashfa
ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Pia, wamependekeza kufikishwa mahakamani viongozi wote wakuu waliokuwa wakishirikiana na mawaziri hao katika ngazi za uamuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkurugenzi
Mtendaji wa PINGO’s Forum, Edward Porokwa alisema wanaipongeza Kamati
ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kufanya kazi kwa uadilifu
na uzalendo, lakini akasema kung’olewa kwa mawaziri hao hakutoshi.
“Tunapendekeza baada ya kuundwa Tume ya
Kimahakama, iwahoji tena mawaziri walioondolewa Dk Emmanuel Nchimbi, Dk
Mathayo David, Shamsi Vuai Nahodha na Balozi Khamis Kagasheki,” alisema
Porokwa.
Porokwa alisema ofisi yake iko tayari kushirikiana
na tume ya kimahakama, kuwaunganisha na wafugaji walioporwa mifugo,
waliobakwa na waliojeruhiwa.
“Tunaamini kamati (ya Bunge), imefanya kazi nzuri
sana na taarifa yao ina ushahidi hadi wa simu zilizotumika kutumwa fedha
za rushwa. Huu tunaamini ni mwanzo tu wa kutambua maovu, mauaji,
ubakaji na mateso waliopata wafugaji,” alisema Porokwa.
Alisema wanatarajia wafugaji na wananchi wengine walioathirika na operesheni hiyo, watalipwa fidia stahiki.
Ofisa Miradi wa Shirika hilo, Isaya Naini alisema
Operesheni Tokomeza imevuruga uhusiano wa muda mrefu baina ya wafugaji
na hifadhi, kwani mamia ya wafugaji ambao ni walinzi wa hifadhi
wameathirika
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment