Home » » Tibaijuka aombwa kuingilia kati mzozo NHC

Tibaijuka aombwa kuingilia kati mzozo NHC

WAPANGAJI wa Shirika la Nyumba Tanzania eneo la Serengeti View kata ya Levolosi jijini Arusha wamemtaka Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka kuingilia kati mgogoro baina ya wapangaji hao na meneja wa shirika hilo mkoa wa Arusha.
Mgogoro huo umeibuka baada ya meneja wa mkoa  wa shirika la nyumba kuwaandikia barua wapangaji hao kuwataka kuanzia mwezi ujao walipe kodi ya ongezeko la asilimia 133.29 kinyume na mikataba yao inavyosema.
Mwenyekiti wa kamati maalumu ya wapangaji hao, Emanuel Mulilo, alisema kama wapangaji wa shirika wana haki za msingi kwa mujibu wa mikataba waliyoingia na shirika hilo.
Alisema mikataba yao inaelekeza kuwa shirika linaweza kupandisha kodi kwa asilimia 15 kila mwaka baada ya kuwa imefanya marekebisho makubwa ya uboreshaji wa nyumba zake.
“Hapa kuna wapangaji ambao wana miezi mitatu, wengine miezi sita na wengine wana miaka zaidi ya 10 lakini meneja ameandika barua kwa wapangaji wote kuwataka hadi mwisho wa mwezi huu kulipa kodi mpya yenye ongezeko la asilimia 133.29,’’ alisema Mulilo.
Alifafanua kuwa kuna wapangaji wanalipa kodi ya sh 45,000 kwa mwezi lakini sasa wanatakiwa kulipa sh 125,080 kuanzia mwezi ujao kitendo ambacho kinakiuka mikataba.
Kwa mujibu wa nyongeza mpya nyumba zenye ukubwa wa mita za mraba 40 zitatozwa sh 2650 kwa kila mita ya mraba moja hivyo kwa mita 40 za mraba wapangaji watatakiwa kulipa sh 125080 kwa mwezi.

Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa