na Grace Macha, Arusha
SHIRIKA
la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) limeandaa tuzo maalumu kwa waandishi wa
habari nchini wanaoandika habari bora na nzuri kwa ajili ya kuhamasisha utalii
wa ndani na umuhimu wa uhifadhi endelevu.
Meneja
Uhusiano wa shirika hilo, Pascal Shelutete, alisema juzi kuwa shindano hilo
litajumuisha makala zilizotoka magazetini, vipindi vilivyoandaliwa radioni na
kwenye runinga vilivyofanyika kuanzia Januari mosi mpaka Desemba 31 mwaka huu.
Alisema
kwenye mshindi wa kwanza kwenye kila kundi kati ya makundi sita ya kwanza
atapata fedha taslimu sh milioni 1.5, cheti, ngao na safari ya mafunzo ya zaidi
ya siku saba kwenye moja ya nchi za Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Africa (SADC).
Shelutete
alisema washindi wa pili watapata fedha taslim sh milioni moja na ngao wakati
washindi watatu watapata fedha taslim sh 500,000 na cheti ambapo washindi 18
wanatarajiwa kupatikana kwenye habari za uhifadhi na tisa wengine kwenye
uhifadhi wa utalii wa ndani.
Alisema
TANAPA imeamua kutoa tuzo hizo ili kuongeza hamasa kwa waandishi kuandika
habari zitakazowahamasisha wananchi kutembelea vivutio vilivyopo nchini, ili
kukuza utalii wa ndani kwani kwa sasa wanaoongoza kutembelea hifadhi ni watalii
kutoka nje ya nchi.
Shelutete
alisema pia shindano hilo limelenga kutoa elimu zaidi kwa wananchi kupitia
vyombo vya habari kuona umuhimu wa kulinda na kuhifadhi maeneo yaliyotengwa kwa
ajili ya kuhifadhiwa kwa kuepuka kuyavamia au kuingiza mifugo kwa manufaa yao
na taifa kwa ujumla.
Alisema
waandishi wanaotaka kushiriki shindano hilo wanaweza kutembelea mtandao wa
shirika hilo www.tanzaniaparks.com na kujaza fomu maalum kisha wataituma kwa
mkurugenzi mkuu wa TANAPA kupitia meneja uhusiano.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment