Home » » TISA WAJERUHIWA KWENYE MAPIGANO LONGIDO

TISA WAJERUHIWA KWENYE MAPIGANO LONGIDO



na Ramadhani Siwayombe, Arusha
MAPIGANO mapya yaliyoibuka kati ya wafugaji wa jamii ya Kimasai na wa Kiarusha katika kijiji cha Engarenaiboi wilayani Longido, yamesababisha watu tisa kujeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitalini.
Mapigano hayo yaliibuka juzi kutokana na mgogoro wa malisho uliokuwa ukiendelea kati ya pande hizo mbili katika eneo la mpaka wa wilaya za Longido na Arumeru katika kijiji cha Kiseriani.
Mgogoro huo unatokana na wafugaji wa Kiarusha wenye asili ya wilaya ya Arumeru wanaoishi katika kijiji cha Kiseriani kilichoko wilaya ya Longido kuhitilafiana juu ya eneo la malisho ya mifugo na wafugaji wa Kimasai wa asili ya Longido.
Akizungumzia mgogoro huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema baada ya wao juzi kwenda kutatua mgogoro wa Kiseriani kwa kuwasihi wafugaji hao kuacha dhana ya ubaguzi waliyoianzisha kati yao, ndipo kukazuka tena mapigano katika kijiji cha Engarenaibor.
Mulongo alisema baada ya kupata taarifa za kuzuka kwa mapigano hayo walituma askari na walifanikiwa kudhibiti mapigano hayo na kukuta tayari watu hao tisa wamejeruhiwa.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa wito kwa jamii hizo kuacha tabia wanayotaka kuianzisha ya kutengana kwa ukabila, kwani itawaathiri kwa kuwa wana tabia ya kuhama kufuata malisho.
“Nimewaambia wasipoacha dhambi hiyo ya kubaguana wao ndio watakuwa waathirika wakubwa wa dhambi hiyo kwa kuwa ndio wako katika mikoa mingi hapa nchini wakifuata malisho hivyo kama huko waliko nako wenyeji wakiamua kuwafukuza baada ya kutambua ubaguzi wao wataishije na wamenielewa,” alisema Mulongo.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa