Home » » JOSHUA NASARI AOMBA ASKARI WAWAACHIE WAFUASI WAKE

JOSHUA NASARI AOMBA ASKARI WAWAACHIE WAFUASI WAKE


Na Woinde Shizza,Arumeru
 
MSIMAMIZI wa tume ya uchaguzi katika jimbo la Arumeru mashariki,Trasias Kagenzi  amemtangaza ,Joshua Nasari (26)wa CHADEMA,kuwa mbunge mteule katika jimbo hilo baada ya kuibuka kidedea na kuwabwaga wenzake saba kutoka vyama mbalimbali vilivyoshiriki uchaguzi huo.
 
Akitangaza matokeo hayo leo(jana) alfajiri ,Kagenzi alisema kuwa Nasari aliibuka mshindi kwa kupata kura 32,972 sawa na asilimia 54,na kufuatiwa na mgombea wa chama cha mapinduzi ,Sioi Sumari aliyeambulia kura 26,757 sawa na asilimia 42.
 
Aidha aliongeza kuwa jumla ya wapiga kura waliojiandikisha katika jimbo la uchaguzi la  Arumeru mashariki walikuwa ni 127,453,waliopiga kura ni 60,696 ,kura halali zilikuwa 60,036 ,zilizoharibika ni 661.
 
Kagenzi alisema kuwa vyama vingine vilivyoshiriki ni AFP ambapo mgombea wake alipata kura 139,UPDP kura 18,TLP kura 18,SAU 22,NRA 35  na DP kura 77,hata hivyo alifafanua kuwa hali ya uchaguzi ilienda vizuri kwani hakukuwapo na malalamiko mengi katika kipindi cha kampeni hadi kupiga kura ,ambapo wakazi mbalimbali walijitokeza na kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.
 
Msimamizi huyo mara baada ya kutangaza matokeo hayo alivishukuru vyama vya siasa vilivyoshiriki kinyang’anyiri hicho cha uchaguzi, akidai vimeonyesha ukomavu wa hali ya juu licha ya ya kasoro na dosari ndogo ndogo zilizojitokeza na kutoa wito kwa vya vya siasa kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi la upigaji kura ili kuondoa malalamiko pindi mshindi anapotangazwa kwa madai kuwa matokeo yamechakachuliwa.
 
Alivitaka vyama vya siasa kuiamini tume ya uchaguzi kwani hatua ya kuchelewesha matokeo hatokei maksudi kwa lengo la kutoa ushindi wa mezani kwa vyama vingine ila kinachofanyika ni taratibu za kuhakiki masanduku ya kura pamoja  na fomu za mawakala,hiyo aliwasihi wafuasi wa vyama vya siasa kuacha kuitumia lawama ofisi ya msimamizi wa uchaguzi na kutishia kumvamia kwa lengo la kushinikiza matokeo yatangazwe haraka.
 
‘’wafuasi wa vyama ni vema wawe wavumilivu kwani hatua ya kupiga kelele na kutaka wapatiwe matokeo haraka ,yanakuwa hayana maana kwani utaratibu wa sasa tunatumia vyombo vya kisasa katika kuhakiki matokeo kwa kutumia kompyuta ‘projector’alisema Kagenzi
 
Akizungumza muda mfupi baada ya kutangazwa matokeo hayo,Nasari pamoja na kuwashukuru wapiga kura wake kwa kumchagua ,aliipongeza tume ya uchaguzi kwa kusimamia vema uchaguzi huo kwani hali hiyo imeondoa malalamiko mengi na  pengine yangewea kuibua machafuko na uvunjivu wa amani.
 
Nasari alisema kuwa kazi iliyombele yake ni kuhakikisha anarudisha fadhila kwa wapiga kuwa wake ambao wamemwamini na kuamua kumchagua kwa kuwatumikia ,ambapo alitangaza kuanza kazi mara moja ya kuchimba visima viwili katika kata Maroroni ambako kuna shida kubwa ya uhaba wa maji.
 
Katika hatua nyingine Nasari alitaka jeshi la polisi kuwaachia huru wafuasi wa chadema zaidi ya 70 anaoamini  ni wapiga kura wake, wanaoshikiliwa katika kituo kikuu cha Arusha kutokana na vurugu zilizozuka eneo la mji mdogo wa Usa River baada ya wafuasi wa chadema kuzingira barabara na kuzuia magari kuingia eneo la kuhesabia kuwa na kusababisha  kupigwa mawe na kuvunjwa vioo kwa gari la kifahari la  naibu kamishina wa jeshi la polisi nchini ,Isaya Mgulu,lenye namba za usajiri  T 859 BWB.
 
Katika vurugu hizo jeshi la polisi lililazimika kuwatawanya wafuasi hao kwa kuwafyatulia mabomu ya machozi majira saa 3 usiku hadi saa 5 ,ambapo polisi iliamua kutumia sialaha za moto na mabomu kuwatawanya wafuasi hao waliokuwa na jazba wakizuia gari la aina yoyote kupita na kwenye eneo la chumba cha majumuisho wakidai yanapitisha kura chafu kwa lengo la kuchakachua matokeo.
 
Polisi ilifanikiwa kuwatia mbaroni wafuasi zaidi 70 wa chadema na  wanashililia katika kituo cha polisi mjini Arusha ,hadi (leo)jana  asubuhi walikuwa bado wakiendelea kutoa maelezo kituoni hapo.
Habari kwa hisani ya Michuzi Blog

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa