Home » » CHADEMA Waanza Kutumia Helkopita katika kampeni Arumeru

CHADEMA Waanza Kutumia Helkopita katika kampeni Arumeru



Neville Meena na Mussa Juma, Arumeru
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilianza kutumia helkopta katika kampeni zake za kumnadi mgombea wake wa ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.

Habari ambazo gazeti hili limezipata zinasema helkopta hiyo itaendelea kutumika hadi siku ya mwisho ya kampeni na kwamba itakiwezesha chama hicho kufanya mikutano kati ya mitano hadi minane kwa siku.

Mkuu wa Operesheni wa uchaguzi wa Chadema katika jimbo hilo, John Mrema alisema kuanza kutumika kwa helkopta hiyo kutamwezesha mgombea wao kufanya mikutano mitano kwenye kata tano tofauti.

Mikutano ya jana ilifanyika katika vijiji vya Ngurdoto Kata ya Maji ya Chai, Ngabobo Kata ya Ngarenanyuki, Kijiji cha Sakila Kata ya Kikatiti na vijiji na kata za King’ori na Nkoanrua.

Helkopta hiyo ilianza kuonekana katika anga la Usa River, Arumeru jana asubuhi na hakukuwa na taarifa za awali kuhusu ujio wake kama ambavyo chama hicho kimekuwa kikifanya katika kampeni nyingine zilizotangulia.

Helkopta hiyo yenye maneno makubwa CHADEMA, ilitumika wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho zilizofanyika katika Uwanja wa Shule ya msingi Leganga, Usa River Machi 10 mwaka huu na tangu wakati huo haikuwahi kuonekana tena hadi jana.

Dk Slaa na ardhi

Katikamikutano ya jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alimshambulia Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Gudluck Ole Medeye kwamba anahusika na kukodisha shamba la Valesca lililo Jimbo la Arumeru Mashariki kwa wawekezaji kwa bei ya kutupa.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Ngabobo, Ngurdoto na Sakila, Dk Slaa alisema ni aibu mawaziri wa Serikali ya CCM kuomba kura katika Jimbo la Arumeru Mashariki huku wakiwa ni waasisi wa mpango wa kugawa ardhi ya umma kwa walowezi wa kizungu.

Alisema Naibu Waziri huyo, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kabla ya kukubali kutolewa shamba hilo lenye zaidi ya ekari 400 ambalo Serikali itapata kiasi cha Sh2.4 milioni tu kwa mwaka walipaswa kuwakumbuka wananchi.

“Hivi kweli nyie wananchi wa Meru hamuhitaji ardhi hii na mngeshindwa kulipa Sh6000 kwa ekari moja ili muweze kulima, kama alivyouziwa mzungu? ”alihoji Dk Slaa.

Aliwataka wakazi wa jimbo hilo, kukubali mabadiliko sasa kwa kuchagua mbunge wa upinzani ili aweze kuhoji ardhi ya Meru ambayo kiasi kikubwa kimegawanywa kwa walowezi kutoka nje ya nchi.

Vituo bandia

Wakati hayo yakiendelea, tuhuma kwamba kuna vituo 55 vya bandia vilivyoandaliwa kwa lengo la kutumika kuiba kura kwenye uchaguzi huo, zinaonekana kugonganisha vichwa vya maofisa wa uchaguzi.

Tuhuma hizo ni zile zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa juzi kwamba kuna vituo 55 bandia 55 vya kupigia kura katika uchaguzi huo mdogo madai ambayo yalikanushwa na Msimamzi wa Uchaguzi wa Arumeru Mashariki, Trasias Kagenzi.

Juzi Kagenzi alipozungumza na waandishi wa habari alisema vituo halali ambavyo anavitambua ni 327 tu na hakukuwa na kituo ambacho kimeongezwa na kwamba hata kama ikitokea hivyo, itakuwa ni baada ya majadiliano na vyama vyote shiriki.

“Vituo vilivyopo ni 327 pekee, na kama ikitokea kituo kinakuwa na watu zaidi ya 500 ndipo kunaweza kuongezeka, lakini historia inajionesha kila uchaguzi mdogo unapofanyika idadi ya wapigakura inapungua,”alisema Kagenzi.

Lakini jana Kagenzi alikiri kuwapo kwa kasoro kwenye orodha ya vituo hivyo na kwamba alikuwa anawasiliana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ili kuwezesha kufanyika kwa marekebisho.

Maeleo ya Kagenzi yanatokana na ushahidi ambao gazeti hili liliupata kwa kuona orodha ya vituo hivyo, ambayo ilikuwa ikionyesha takwimu mbili tofauti za idadi ya vituo vya kupigia kura.

Katika orodha hiyo, safu ya idadi ya vituo vya kupigia kura katika kata 17 za jimbo hilo ilikuwa ikionyesha vituo 327, wakati safu ya mwisho ya orodha hiyo hiyo ilikuwa ikionyesha kuwapo kwa jumla ya vituo 382, likiwa ni ongezeko la vituo 55.

Waraka wa orodha hiyo unaonyesha kuwa katika Kata ya Akheri kutakuwa na vituo 20 idadi ambayo inayofautiana na iliyotolewa na tume ambavyo ni vituo 18.

Kata nyingine ambazo vituo hivyo vinaonekana kuongezwa ni Kikatiti vituo 22 badala ya 18, Kata ya Kikwe vituo 12 badala ya halali 11, Kata ya Kingori vituo 29 badala ya halali 26 na Kata ya Leguruki vituo 23 badala ya halali 20.

Kata nyingine ni Makiba vituo 21 badla ya halali 18, Majiya chai 24 badala ya 29 halali, Maroroni vituo 21 badala ya 17 halali, Mbuguni vituo 25 badala ya halali 21,Nkoarsambu vituo 10 badala ya 8 vinavyohitajika na Kata ya Ngarenanyuki ambako vimeongezwa vituo sita kutoka halali 20 hadi 26.

Orodha hiyo ambayo Kagenzi alithibitisha kwamba ilikuwa na makosa pia ina kasoro katika Kata za Nkoaranga ambako vituo vimeongezwa kutoka halali 17 hadi 22, Pori kutoka vituo halali 16 hadi 20, Nkwandua kutoka vituo 22 hadi kufikia 25 na Kata ya Seela - Sing’isi vituo hivyo viliongezwa kutoka halali 12 hadi 15.

Kata nyingine ni Songoro nyumbani kwa Mgombea wa Chadema, Joshua Nassari vipo vituo 15 na hakuna kilichoongezeka huku Kata ya Usa River ilikuwa na vituo 36, lakini vimeongezeka vitano na kufikia 41.

Kagenzi alisema alipowasiliana na idara ya teknolojia ya habari ya NEC kuhusu kasoro hizo walimwambia kwamba orodha ya awali haikuwa toleo la mwisho na kwamba wangefanya marekebisho ya kuondoa kasoro hizo.

“Wameniambia kwamba hiyo orodha ilikuwa ni working draft tu (rasimu ya kufanyiwa kazi), kwahiyo nimeomba hiyo orodha kamili ya mwisho, wakishanitumia nitaisambaza kwa vyama husika,”alisema Kagenzi jana.

Baadaye msimamizi huyo wa uchaguzi alisema wataalamu kutoka NEC walitarajiwa kuwasili Arumeru jana mchana kwa ajili ya kurekebisha kasoro hizo pamoja na kufanya maandalizi mengine kwa ajili ya uchaguzi huo mdogo.

Hata hivyo, kauli ya Kagenzi ilikuwa ikipishana na ile iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Mallaba ambaye awali alisema hakukuwa na vituo vya nyongeza kama ilivyodaiwa na Dk Slaa.Soma zaidi www.mwananchi.co.tz

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa