Arusha
Home » » BALOZI SEIF ASISITIZA HIFADHI YA JAMII

BALOZI SEIF ASISITIZA HIFADHI YA JAMII

MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema mpango wa serikali ya Tanzania wa hifadhi ya jamii ndio msingi wa sera ya kuondoa umaskini miongoni mwa watu wake ili kulifanya taifa kuwa la kipato cha kati ifikapo 2025.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mkutano mkubwa wa kimataifa wa hifadhi ya jamii, ulioandaliwa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na wadau wengine kwa lengo la kubadilishana uzoefu juu ya nini cha kufanya kusaidia makundi maalumu katika jamii.
Balozi Seif alisema kwa kuzingatia nia ya serikali ya kuwa taifa lenye kipato cha kati mwaka 2025, serikali inaona haja ya kuangalia sera ili iweze kutoa haki kwa makundi yote kuelekea ustawi wa jamii ifikapo mwaka huo.
Alitaka washiriki kuangalia ukusanyaji wa takwimu kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii, kwani kwa hali ilivyo sasa ukusanyaji huo si mzuri na unazuia maendeleo na uimarishaji wa huduma za jamii.
Alisema ipo haja ya kuboresha mazingira ya utawala ili kuwezesha kuimarisha hifadhi kwa wale waliokwishaipata, kubadili sheria ili kuwaingiza na wale ambao hawajapata huduma za hifadhi ya jamii.
Mkutano huo wenye washiriki zaidi ya 150, unashirikisha watengeneza sera, watafiti na waendeshaji wa mifuko ya hifadhi kutoka Kenya, Uganda, Bangladesh, Msumbiji, Lesotho, Malawi, Afrika Kusini, Ghana, Ethiopia, Zambia, Sudan Kusini na wenyeji Tanzania.
Mkurugenzi Msaidizi Mkuu wa Shirika la Kazi duniani (ILO) na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika, Aeneas C. Chuma, alisema Umoja wa Mataifa umefurahishwa na kuwapo kwa kongamano hilo, kwani suala la hifadhi ni msingi wa maendeleo katika uchumi wowote endelevu.
Mkutano huo wa siku tatu unafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC)
Chanzo:Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa