UNESCO Yaunga Mkono Juhudi za Serikali Kuboresha Mfumo wa Usimamizi wa Mafunzo Endelevu ya Walimu (MEWAKA)

Picture1

Picture2

Picture3

Picture4

Picture5

Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeonyesha dhamira ya dhati Kufanya kazi bega kwa bega na wadau wa maendeleo kuhakikisha uboreshaji wa mfumo wa usimamizi wa mafunzo endelevu wa walimu kazini yaani MEWAKA unaboreshwa na kukamilika kwa wakati na kwa ufanisi ili kuwezesha mahitaji ya walimu wa Sekondari.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha warsha  iliyofanyika kwa muda ya siku mbili ya tarehe 28 na 29 Agosti 2025, ya mapitio ya mfumo wa MEWAKA ulioboreshwa Mratibu wa Mradi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi. Lina Rujweka, alitoa shukrani kwa juhudi na muda uliowekezwa na wadau wote, ikitambua mchango wao muhimu unaotarajiwa kuleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mradi huu hasa UNESCO na Jamhuri ya Korea kupitia mradi wa ‘’KFIT III wa Transforming Education through ICT in Africa’’ kwa kuendelea kutoa msaada wa kifedha.

Shirika la UNESCO Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), inaendelea na juhudi za uboreshaji mfumo wa MEWAKA ili kuzingatia mahitaji ya walimu wa shule za sekondari.

Ushirikiano huu ulitokana na tathmini ya mahitaji iliyoonyesha kuwa mfumo wa sasa ulikuwa umeundwa mahsusi kwa ajili ya kuwa jukwaa la mafunzo ya maendeleo ya kitaaluma kwa walimu wa shule za msingi.

Hivyo, wadau walikutanishwa ili kupitia toleo la awali la mfumo wa MEWAKA kwa lengo la kuhakikisha umuhimu, ubora, na uendelevu wa muda mrefu wa jukwaa hilo.

Wadau hao walikuwa kutoka  wizara ya elimu, sayansi na Teknolojia , Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Taasisi ya Elimu Tanzania, Tume ya Kitaifa ya UNESCO na baadhi ya walimu wa shule za sekondari.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ally Mape alisema majukwaa ya kidijitali ni nyenzo yenye nguvu ya maendeleo ya kitaaluma, yanayochangia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha walimu kupata ujuzi na kujiamini ili kufanikisha kazi zao katika Dunia ya sasa.

Kwa upande wake mkuu wa Sekta ya Elimu kutoka Ofisi ya UNESCO Dar es Salaam, Dkt. Faith Shayo, ameeleza kuwa lengo kuu ni kupanua upatikanaji wa mafunzo endelevu ya kitaaluma kupitia majukwaa ya kidijitali, hivyo itasaidia kuboresha matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji kote nchini.

Hata hivyo Dkt. Shayo aliwahimiza wadau kutoa maoni na mitazamo yao kusaidia kuhakikisha toleo la mwisho la mfumo huu sio tu kuwa la kisasa bali pia rahisi kutumia na lenye matokeo chanya.

Mpango huu unalingana na juhudi za Serikali za kuunganisha TEHAMA katika elimu, kama inavyoonekana katika sera na mikakati muhimu ya kitaifa ikiwemo Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023, Mkakati wa Kitaifa wa Elimu ya Kidijitali 2025 – 2030, Dira ya Maendeleo ya 2050, Mitaala ya Elimu ya Msingi na ya Ualimu, pamoja na mipango ya kimataifa kama vile Malengo ya Maendeleo Endelevu hasa lengo namba nne.


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

RC Kihongosi Asikiliza na Kutatua Kero za Wamiliki na Wafanyakazi wa Saluni, Jijini Arusha.

WhatsApp%20Image%202025-07-23%20at%2007.58.16

WhatsApp%20Image%202025-07-23%20at%2007.58.14

WhatsApp%20Image%202025-07-23%20at%2007.57.14

WhatsApp%20Image%202025-07-23%20at%2007.57.12


Na Frida Maganga,Arusha 

Watumishi na waajiriwa wa Halimashauri ya jiji la  Arusha wametakiwa kufanya kazi zao kwa mujibu wa taratibu na sharia pamoja na miongozo yao ya kazi pasipo kutengeneza mazingira yoyote yale ya kumwonea mwanachi yoyote yule mkazi wa mkoa wa Arusha .


Rai hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Arusha Bwana Kenani Kihongosi wakati akizungumza na wamiliki na watumishi wa Salooni kike na kiume jijiini Arusha  wakati akijibu malamiko ya mmiliki wa saluni Bi Rose Barage.


Ambapo Bi. Rose aliamueleza mkuu mkoa kuhusiana na manyanyaso anayo yapata pamoja kutoka kwa mtu aliyetambulika kwa jina la Lusekelo anayetambulika kama mmiliki aliyekodisha chumba cha biashara halimashauri ya jiji la Arusha na Kumpangishia yeye kwa bei kubwa.


Kutokana malalamiko hayo mkuu wa mkoa Mhe. Kihongosi alimwagiza mkurugenzi wa jiji la Arusha kuhakikisha wanampatia siku hii ya leo mkataba Bi. Rose ili aondokane na manyanyaso .

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

NBC Yakutana na Wateja Wake Wakubwa wa Jijini Arusha, Yajadili Fursa, Ufanisi wa Huduma Zake Kwa wateja.

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekutana na wateja wake wakubwa kutoka kampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) wa jijini Arusha ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya za benki hiyo sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Benki hiyo pia ilitumia fursa hiyo kujadili na wateja hao namna inavyoweza kuboresha huduma zake kulingana na mahitaji yao.

Katika kufanikisha hilo, jana benki hiyo kupitia timu yake ya Biashara na Uwekezaji (CIB) iliandaa hafla maalum ya chakula cha jioni iliyofanyika jijini humo ikiongozwa na Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa benki hiyo Bw, Elvis Ndunguru sambamba na maofisa wengine waandamizi wa benki hiyo kutoka makao makuu na matawi yake ya jijini Arusha.


Akizungumza kwenye hafla hiyo Bw Ndunguru alisema tukio hilo ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuendelea kuwa karibu zaidi na wateja wake kwa nia ya kutambulisha huduma zake mpya ikiwemo huduma ya NBC Connect mahususi kwa kundi hilo la wateja, kupata mrejesho wa huduma hizo kutoka kwa wateja hao sambamba na kutoa fursa kwa wateja kubadilishana fursa za biashara.

“Tukiwa kama muhimili muhimu wa utoaji wa huduma za kifedha nchini, NBC tunatambua umuhimu wa utoaji wa huduma bora kwa wateja na kukuza ushirikiano kati yetu na wateja wetu. Hii inasababishwa na mabadiliko yanayotokana na ubunifu na maendeleo ya kiteknolojia tunayoyafanya kila siku’’

“Hivyo hatua hii ya kukutana na wateja wetu wakubwa inatoa fursa kwetu kuelezea maboresho makubwa tuliyofanya kwenye huduma zetu hivi karibuni sambamba na kutambulisha huduma mpya zilizorahisishwa zaidi kidigitali na zinazoendana na mahitaji ya wateja wetu.’’ Alisema

Aidha, kupitia mpango huo benki hiyo imekuwa ikielezea mikakati yake mipana inayolenga kuwahudumia kwa ufanisi zaidi wateja hao, kuwajengea mitandao ya kibiashara miongoni mwao sambamba na kuwasogezea huduma za kibenki karibu zaidi huku huduma ya NBC Connect ikitajwa kama suluhisho muhimu katika kuwasogezea huduma za kibenki wateja hao wakubwa yakiwemo mashirika na kampuni binafsi, pamoja na taasisi za serikali.

“Tunaamini kuwa msingi wa huduma za kipekee ni kuelewa mahitaji na matakwa ya wateja wetu, matukio kama haya yanatupatia mitazamo au maono yanayotusaidia kuwa wabunifu zaidi na kuboresha uzoefu wa kibenki kwa ujumla.” Aliongeza Bw Ndunguru.

Aidha, Bw Ndunguru alitaja baadhi ya mambo muhimu ambayo benki hiyo imekuwa ikiyazingatia katika kukuza ushirikiano na taasisi za kibiashara hapa nchini kuwa ni pamoja na utoaji wa suluhisho zenye ubunifu katika huduma za kifedha, Ubunifu wa kiteknolojia, Ubia wa kimkakati, Kukuza Ukuaji wa Uchumi pamoja na Uwajibikaji kwa jamii huku kipaumbeke kikiwekwa zaidi kwenye masula ya Elimu, Afya na uhifadhi wa mazingira.

“Hivyo basi NBC tunazialika jumuiya za wafanyabiashara kuangalia fursa na faida za kushirikiana na taasisi hii ya fedha ambayo ina dhamira ya dhati na mafanikio yao, kwa kukuza ushirikiano na kutoa zana zinazohitajika katika ukuaji. NBC inalenga kuwa mshirika mwaminifu anaayetegemewa katika biashara hapa nchini,’’ alibainisha.

Wakizungumzia hatua hiyo baadhi ya wateja wa benki hiyo mkoani Arusha walisema imekuja wakati muafaka hasa katika kipindi hiki ambacho mkoa huo upo kwenye mapinduzi makubwa ya kiuchumi kutokana ustawi mkubwa wa sekta ya utalii ikiwa ni matunda ya jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mkakati wake wa Royal Tour.

“Kwa sasa mkoa wa Arusha tupo kwenye kasi kubwa ya mabadiliko ya kiuchumi yanayochagizwa na ukuaji wa sekta ya utalii, biashara, kilimo na viwanda. Ni habari njema kwetu kuona kwamba benki ya NBC ambayo inatuhudumia wadau wengi kwenye sekta hizi inatuunga mkono kupitia huduma zao za kisasa ikiwemo zile za kidigitali ambazo kiukweli zimekuwa msaada mkubwa hususani kwenye huduma za miamala ya kifedha na makusanyo ya serikali,’’ alisema Bw Abdallah Kiwango kutoka Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).


Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw, Elvis Ndunguru (kushoto) akizungumza na wageni waalikwa ambao ni wateja wa benki hiyo jijini Arusha wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wakubwa kutoka makampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Hafla hiyo iliyoandaliwa kupitia timu ya Biashara na Uwekezaji (CIB) ya benki hiyo ilifanyika jana jioni jijini Arusha.


Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw, Elvis Ndunguru (kulia) akibadilishana Mawazo na baadhi ya wateja wa benki hiyo jijini Arusha wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wakubwa kutoka makampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Hafla hiyo iliyoandaliwa kupitia timu ya Biashara na Uwekezaji (CIB) ya benki hiyo ilifanyika jana jioni jijini Arusha.





Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw, Elvis Ndunguru (katikati aliesimama) akisalimiana na baadhi ya wateja wa benki hiyo jijini Arusha wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wakubwa kutoka makampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Hafla hiyo iliyoandaliwa kupitia timu ya Biashara na Uwekezaji (CIB) ya benki hiyo ilifanyika jana jioni jijini Arusha.






Baadhi ya wateja wa benki ya NBC jijini Arusha wakifuatilia hafla hiyo







Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw, Elvis Ndunguru (kulia) sambamba na maofisa wengie wa benki hiyo wakizungumza na wageni waalikwa ambao ni wateja wa benki hiyo jijini Arusha wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wakubwa kutoka makampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Hafla hiyo iliyoandaliwa kupitia timu ya Biashara na Uwekezaji (CIB) ya benki hiyo ilifanyika jana jioni jijini Arusha.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

DKT. KIKWETE: NCHI ZA AFRIKA ZINAHITAJI KUWEKEZA ZAIDI KATIKA TAFITI NA KILIMO

Na.Vero Ignatus ARUSHA

Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na Umasikini umefanyika Jijini Arusha kwa lengo la Kuwaunganisha wataalamu wa utafiti na watunga sera,ambapo nchi za Afrika zikisisitizwa kuona kwamba ipo haja kuwekeza nguvu katika kilimo ili kuondokana na umaskini sambamba na kufanya tafiti za kilimo

Hayo yamesemwa na Rais Mstaafu Rais wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete leo June 12,2025 wakati wa ufunguzi wa mkutano huo ulioandaliwa na Usimamizi wa Sera ya Oxford (OPM) kwa kushirikiana na data na ushahidi wa kumaliza umaskini uliokithiri (Deep) mapambano dhidi ya umaskini yanahitaji mshikamano wa kitaifa na kimataifa kwani mamilioni wanamahitaji ya msingi kama chakula, elimu na huduma za afya

'' Miaka mitano kuelekea mwisho wa mwaka 2030 katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa bado tupo nyuma lakini hii ni kwa sababu ya shida iliyopatikana katika miaka mitano iliyopita, pamoja na janga la ulimwengu la Covid-19, vita vya jiografia na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa,"

Dkt. Kikwete amesema nchi za Afrika zinahitaji kuwekeza zaidi katika utafiti na kilimo, ikiwemo kuwekeza nguvu zaidi kwenye kilimo ambacho ni njia pekee ya kuondoa umaskini kwa haraka na kuwawezesha vijana kupata mwelekeo ujao wa maendeleo kwa nchi hizo.

Sambamba na hayo alisema alama mpya ya kupima umaskini uliokithiri, ambao sasa umerekebishwa kutoka dola za marekani USD 1.25 uliopita kwa siku, hadi kufikia dola 3.00 kwa siku lakini bado kunachangamoto ya kupunguza umaskini kwa watu mbalimbali kwa kuhimiza kilimo na mapato ya watu kuongezeka kasi ya uchumi na kimaendeleo.

Dkt.Kikwete amesema malengo ya 2030 ya SDG ya kupunguza umasikini hayawezi kupatikana kwa wakati na kwamba hata kiwango cha kipimo cha umaskini kinahitaji kubadilishwa kwani wanodhaniwa kuwa wanaishi katika umaskini uliokithiri sasa wanaelezewa kuwa wale wanaoishi chini ya USD 3.0 kwa siku na kuongeza kuwa Rais kwa awamu yake kwa upande wa Tanzania alijitahidi kuhakikisha anatekeleza dira ya Maendeleo ya mwaka 2050

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Utafiti juu ya kuondoa umaskini (REPOA) Dk.Donald Mmari, alizishauri nchi zote za Afrika kuharakisha marekebisho katika mfumo wao wa kiuchumi na mifumo ya kifedha ili kuwezesha raia wao kuboresha ustawi wao.

Naye Mkurugenzi wa Nchi wa Usimamizi wa Sera ya Oxford (OPM) nchini Tanzania, Dk.Charles Sokile alisema hapo zamani watu wanaoishi chini ya dola 1.25 walizingatiwa kuwa chini ya umaskini mkubwa.

"Lakini kipimo hiki sasa kimepitiwa na kubadilishwa kuwa kiwango cha chini cha dola za marekani 3.0, ambacho ni sawa na Sh,.7,800 kama alama ya kupima umaskini na kuongeza kuwa alama mpya imezingatia mfumko wa bei, mabadiliko ya hali ya hewa, yanayoathiri matokeo ya kilimo na changamoto za kifedha zinazoibuka"

Kwa upande wake, Prof.Ernest Aryeetey mtaalam wa uchumi alisema wakati data zinaonyesha kuwa viwango vya umaskini wa ulimwengu vinapungua kote ulimwenguni,lakini ni vema

serikali zote kwa pamoja zinahitaji mbinu za utafiti ili kupata data na ushahidi katika mikakati ya kupunguza umasikini.

Prof. Ernest pia alitaka uwekezaji katika utafiti ambao unaweza kuja na njia za bajeti zilizowekwa ambazo zinaweza kulenga vizuri zaidi kubainisha mikakati ya upunguzwaji wa umaskini Ubunifu na Ushirikiano.

Aidha ifahamike kuwa Mabadiliko yanahitaji ubunifu, ushirikiano, na matumizi ya maarifa,hili ndilo lengo la mkutano huo na kutoa suluhisho la vitendo na kushirikishana mbinu endelevu. Uchumi unawahitaji watu wote.









Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Dkt. Mpango Azindua Shule ya Sekondari ya Mfano ya Benki ya CRDB, Benki Hiyo Ikitimiza Miaka 30

Arusha 16 Mei 2025 - Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, amezindua rasmi Shule ya Sekondari ya Mfano ya Benki ya CRDB, itayojengwa katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya Benki ya CRDB.

 Shule hiyo ya kisasa ni matokeo ya dhamira ya Benki hiyo ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwekeza kwenye elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shule hiyo uliofanyika katika seimna ya wanahisa wa Benki ya CRDB kuelekea Mkutano Mkuu, Dkt. Mpango aliipongeza Benki ya CRDB kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya kijamii, hususan sekta ya elimu. 
“Nawapongeza kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa sekta binafsi. Mmekuwa mstari wa mbele sio tu kwenye huduma za kifedha bali pia katika kuleta mabadiliko ya kweli kwenye jamii,” alisema Dkt. Mpango huku akiipongeza benki hiyo pia kwa kutimiza miaka 30 tokea kuanzishwa kwake mwaka 1996.

Akizungumza katika semina hiyo ya wanahisa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, Benki ya CRDB imeendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa Taifa kwa kutoa huduma za kifedha zenye kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Shule ya Sekondari ya Mfano ya Benki ya CRDB ina uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 600 na imejengwa kwa viwango vya kisasa ikiwa na madarasa ya kisasa 16, maabara 4, maktaba 1 chumba cha TEHAMA 1, ofisi za walimu na wafanyakazi 11, vyoo 53, miundombinu rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, pamoja na maeneo rafiki ya michezo. Mradi huu unatarajiwa kugharimu takribani shilingi bilioni 5.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela, alisema shule hiyo ni zawadi ya Benki kwa Watanzania katika kuadhimisha miaka 30 ya mafanikio ya benki hiyo. “Tulipojiuliza ni zawadi gani ya kipekee tungeweza kuwapa Watanzania katika kutimiza miaka 30, tulikubaliana kwamba elimu ni urithi wenye nguvu kuliko wote. Shule hii ni ushahidi wa dhamira yetu ya kuwekeza katika kizazi kijacho,” alisema Nsekela.
Nsekela aliongeza kuwa shule hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa Benki ya CRDB wa kurudisha kwa jamii katika nyanja za ya elimu, afya, mazingira na uwezeshaji wanawake kupitia CRDB Bank Foundation. “Tunaamini kuwa maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa bila uwekezaji wa makusudi katika elimu. Kupitia shule hii, tunaweka msingi wa taifa lenye maarifa, maadili na ushindani wa kimataifa,” alibainisha.
Akitoa salamu zake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), aliishukuru Benki ya CRDB kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini. “Kwa niaba ya Serikali na Wizara ya Elimu, naishukuru sana Benki ya CRDB kwa maono na uamuzi huu wa kujenga shule ya kisasa kwa ajili ya watoto wa Kitanzania. Huu ni mfano hai wa jinsi sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na Serikali katika kujenga musatakabali bora kwa watoto na vijana wetu.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Martin Warioba, alisema shule hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Benki ya CRDB kuboresha mazingira ya elimu nchini na kufungua fursa kwa watoto wa Kitanzania. “Mbali na kujenga shule hii ya mfano, tumejipanga pia kuanzisha mpango wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kwa kushirikiana na Wizara ya elimu.”

Uzinduzi wa shule hiyo unachukuliwa kama alama ya mafanikio ya miaka 30 ya Benki ya CRDB, na uthibitisho wa maono yake ya kujenga taifa lenye misingi imara ya elimu, usawa na maendeleo endelevu. “Tunajivunia kuona uwekezaji wetu ukiendelea kuzaa faida zaidi katika jamii,” alisema mmoja ya Wanahisa waliohudhuria semina hiyo.
Wanahisa wa Benki ya CRDB watafanya Mkutano Mkuu wa 30 kesho ambapo ajenda mbalimbali zinatarajiwa kujadiliwa ikiwamo kuidhinisha pendekezo la bodi ya wakurugenzi la gawio la shilingi 65 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 kulinganisha na gawio la shilingi 50 kwa hisa lililotolewa kwa mwaka 2023.





Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KULETA SERIKALI KWA WANANCHI ILI KULETA MAENDELEO - MHE. MCHENGERWA




Na John Mapepele

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kwa dhati kuisogeza Serikali karibu zaidi na wananchi wake hasa wale walio na kipato cha chini katika maeneo ya vijijini na mijini ili kuwaletea maendeleo.

Akizungumza kwenye Kongamano la Uchumi la Arusha leo Mei 3, 2025 jijini Arusha akiwa miongoni mwa watoa mada, Mhe. Mchengerwa amefafanua kwamba lengo kuu ni kuwakomboa wananchi kutoka katika mnyororo wa ukosefu wa taarifa, huduma na fursa, kwa kuwajengea uelewa, uwezo na maarifa ya msingi, sambamba na kuwawekea miundombinu inayowawezesha kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza mipango yao ya maendeleo.

“Tupo katika zama ambazo maendeleo hayategemei tena maamuzi ya viongozi wa kitaifa peke yao, bali yanategemea uwezo wa maeneo yetu ya mikoa na halmashauri zetu kuongoza kwa dira, maarifa na maamuzi ya kimkakati”.Amefafanua Mhe. Mchengerwa 
Aidha, amesema utawala bora siyo tu matumizi ya sheria bali ni falsafa ya kuwezesha kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika ndoto ya taifa na kujenga taasisi imara, kusimamia rasilimali kwa uadilifu, na kutoa huduma kwa usawa bila upendeleo.

Amesisitiza kuwa kwa kutumia sera ya Decentralization by Devolution (D-by-D), halmashauri zimewezeshwa kupanga na kutekeleza mipango yao kulingana na vipaumbele vya wananchi wao na kwamba hiyo ndio njia ya kweli ya kukuza demokrasia ya kiuchumi.

”Kwa maana hiyo, TAMISEMI imewapa halmashauri zetu nguvu ya kufanya maamuzi kwa mujibu wa mazingira ya jamii zao. Hili linawezesha uwekezaji wa ardhi, huduma bora kwa wananchi, na kuimarisha mapato ya ndani”. Ameongeza Waziri Mchengerwa 

Akifafanua zaidi amesema ustawi wa mikoa hautatokana na maazimio ya makaratasi pekee, bali na uthubutu wa viongozi wake kuondoa matabaka baina ya walionacho na wasio nacho ambapo amesisitiza mikoa ina wajibu wa kufanya tafiti za kina za fursa zilizopo, kutambua changamoto kisekta, kutafuta majawabu yanayotekelezeka na kuanzisha ubia mtambuka (multi-sectoral partnerships) kwa kuzingatia dira ya maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Waziri Mchengerwa ameagiza kwamba kongamano lisiwe tu mkutano wa mijadala, bali chemchemi ya fikra mpya, dira ya uwekezaji wenye tija, na mlango wa fursa kwa kila raia wa Mkoa wa Arusha iwe ni kijijini au mijini.

Ametaka ongamano hilo liwe chachu ya kufungua milango mipya ya uwekezaji kwa kushirikisha Wizara na Taasisi zote husika za Serikali ili kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji yanaboreshwa kwa wepesi, uwazi na ushawishi chanya.

Maeneo yaliyotambuliwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya uwekezaji yaharakishwe kuhuishwa kwa kupangwa kitaalamu, kupimwa kwa usahihi, fidia zote itolewe kwa haki, na miundombinu ya msingi (barabara, maji, umeme, mawasiliano na huduma nyingine) ijengwe kwa haraka.
Amesisitiza kuwa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali washirikishwe kwa kina, kwa uwazi, na kwa heshima pasipo ubaguzi wa hali za kiuchumi, jinsia, mila wala hadhi ya mtu.

Pia mchango wa wananchi wa kawaida unaojumuisha wakulima, wafanyabiashara wadogo, vijana na wanawake lazima uwekwe kikamilifu kwenye mpango unaotokana na Kongamano hili.

Aidha, ameelekeza sheria za nchi zisimamiwe kwa haki, weledi na uadilifu ili kulinda rasilimali za Mkoa na taifa na kwamba tusiruhusu migogoro isiyo ya lazima ififishe ndoto za mamilioni bali, tutumie maarifa ya ndani na teknolojia ya kisasa, kujifunza kutoka kwa uzoefu wa ndani na nje ya nchi, ili kubuni uwekezaji wa kisasa wenye tija na ustahimilivu wa muda mrefu.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MCHENGERWA AWEKA JIWE LA MSINGI JENGO LA JIJI ARUSHA, ASHUHUDIA UTIAJI SAINI MIKATABA YA MIRADI YA BILIONI 40




Na John Mapepele

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa leo ameweka jiwe la msingi kwenye jengo la utawala la jiji la Arusha na kushuhudia utiaji wa saini mikataba ya mradi wa Stendi Kuu ya Mkoa wa Arusha, Soko la Mrombo na Bustani ya Mapumziko ya Themi vyote vikiwa thamani ya takriban shilingi bilioni 40.

Akikagua ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya jiji la Arusha lenye sakafu tisa ambalo litakapokamilika litagharimu bilioni 9.8 amemtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi kwa wakati ili kuondokana na adha ya sasa ya watumishi kufanyia kazi kutokea kwenye ofisi zilizo katika maeneo tofauti hali inayochelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi.

"Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kutoa fedha za ujenzi wa jengo hili kwa kuwa baada ya kukamilika litakuwa mkombozi kwa watumishi" . Amefafanua Mhe. Mchengerwa 

Aidha ameuelekeza uongozi wa Mkoa na Jiji la Arusha kuhakikisha jengo hilo linakamilika mara moja na endapo kutakuwa na mkwamo wowote wachukue hatua.

Amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda kwa kukwamua mgogoro wa kushindwa kukamilika kwa jengo hilo kwa zaidi ya miaka 5 kutokana na masuala ya kisiasa.

Mradi huo umefikia asilimia 62 na unafanywa na mkandarasi mzawa M/S Tribe Construction Ltd na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.

Akihutubia wananchi baada ya kushuhudia utiaji wa saini mikataba ya mradi wa ujenzi wa Stendi Kuu ya Mkoa wa Arusha na Soko la Mrombo na Bustani ya Mapumziko ya Themi, Mhe. Mchengerwa amewataka viongozi kufanya maaamuzi magumu katika kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye. 

Miradi hiyo ambayo inatarajia kugharimu bilioni 30.6 itakapokamilika ametaka iwe inaweza kujiendesha yenyewe na kutoa faida.

Pia amesisitiza kuilinda, na kufanya usafi ili iwezekudumu kwa muda mrefu pindi itakapokamilika.

"Jukumu letu ni kuitunza miundombinu hii itakayojengwa kwa gharama kubwa ili iweze kudumu kwa muda uliotarajiwa. Aidha, naelekeza Halmashauri zenye Miradi yenye kujiendesha kama Masoko na Stendi zihakikishe miradi hiyo inajiendesha na kuzalisha mapato kwenye Halmashauri husika." Amesisitiza Mhe. Waziri 

Amemtaka mkandarasi kufanya kazi kwa haraka na kukamillisha kulingana na mkataba na mpango kazi uliokubalika ili wananchi wa Jiji la Arusha waanze kunufaika na miundombinu hiyo ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza katika jijini Arusha.

Aidha, amemtaka mkandarasi mshauri kuhakikisha mikataba hiyo inasimamiwa kikamilifu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi na TARURA ili ikamilike ndani ya muda uliopangwa, lakini pia katika ubora uliokubalika ili thamani ya fedha ionekane.

Pia amewaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri wasimamie kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo kwa kutumia rasilimali watu na vifaa vilivyopo kwenye Halmashauri husika.
Waziri Mchengerwa amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha maisha ya Wananchi. Mojawapo ya hatua zinazochukuliwa ni kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, Masoko, pamoja utunzaji wa Mazingira katika maeneo ya mijini chini ya Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji ya Tanzania kwa kuhusisha Ushindani ambao kitaalam unajulikana kama Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness (TACTIC) Project.

"Ndugu Wananchi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatekeleza kwa vitendo falsafa ya maendeleo jumuishi. Miradi tunayoizindua leo kupitia Mradi wa TACTIC siyo miundombinu pekee bali ni daraja kati ya leo na kesho bora zaidi kwa wananchi wetu." Amesisitiza


Amesema miradi hiyo inatekelezwa kupitia Mkopo wa Benki ya Dunia utakaogharimu kiasi cha Dola za Kimarekami Milioni 410 na inatekelezwa katika miji 45 mbalimbali nchini. Lengo kuu la mradi wa TACTIC ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa Miji pamoja na kuziwezesha Halmashauri za Miji na Majiji kutoa huduma bora kwa wananchi.


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

KUUNDWA KWA JAB NI HATUA YA KUIMARISHA NA KUBORESHA SEKTA YA HABARI - MAJALIWA


Na Mwandishi Wetu, JAB.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua kadhaa katika kuimarisha na kuboresha sekta ya habari nchini ikiwa ni pamoja na kuunda Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.

Waziri Mkuu amesema hayo leo tarehe 29 Aprili, 2025 wakati akifunga Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari lililofanyika jijini Arusha kwa siku mbili.
“Kwenye sekta ya habari na utangazaji, falsafa ya “4Rs” za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, alizozibainisha baada ya kuingia madarakani mwezi Machi 2021, imetekelezwa kwa vitendo hususani kwenye eneo la “Reforms” (Mageuzi),” amesema Waziri Mkuu na kuongeza;

“Serikali ya Awamu ya Sita katika kutekeleza falsafa hii imechukuwa hatua mbalimbali kuimarisha sekta ya habari na utangazaji nchini kwa kuunda chombo kipya cha kushughulikia usajili wa taaluma ya waandishi wa habari yaani Bodi ya Ithibati”.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari iliyozinduliwa mwaka huu ina jukumu la kusimamia viwango vya kitaaluma kwa wanahabari ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa matakwa ya kisheria chini ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.

Amesema hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni kuhakikisha inawezesha shirika la Habari la utangazaji kuwepo kisheria pamoja na kuimarisha Idara ya Habari Maelezo kwa kununua vitendea kazi vikiwemo Magari na vifaa vya kurushia matangazo mbashara.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inayosema “Uhabarishaji kwenye Dunia Mpya: Mchango wa Akili Mnemba katika uhuru wa vyombo vya habari” inalenga kujadili athari za teknolojia ya akili mnemba katika uendeshaji wa vyombo vya Habari na uhuru wake.

Amesema Serikali katika kuhakikisha Akili Mnemba (AI) inatumika kwa njia inayowezesha badala ya kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari, imeanzisha mchakato wa kuandaa sera maalum ya AI na waandishi wanaowajibu wa kuchangia ili kupata sera nzuri.

“Sera hii itatoa mwongozo wa matumizi ya AI katika vyombo vya habari, ili kuhakikisha kwamba teknolojia mpya zinaendana na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari, uwazi, na uadilifu wa uandishi wa Habari, hivyo mtumie muda wenu hapa kujadili na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha sera hiyo,” amesema Waziri Mkuu.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa