ASKOFU John Lenkishon Kispan wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini Kenya
(ELCK), ameishauri Serikali ya Tanzania kuchukua tahadhari juu ya matukio ya
ugaidi kwa kuimarisha ulinzi katika mipaka yake hasa ule wa Namanga na kutumia
mashine maalumu za kukagua wageni wanaoingia na kutoka.
Askofu Kispan alitoa wito huo jana kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya
alipokutana na Askofu Solom Masangwa wa kanisa hilo nchini, Dayosisi ya
Kaskazini Kati, katika ibada ya usharika wa Namanga, wilayani Longido.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa ibada hiyo, Askofu Kispan alisema matukio
ya ugaidi yanaitesa Kenya kutokana na magaidi kuwaua watu wasio na hatia.
"Nashauri zitumike mashine maalumu za kufanya ukaguzi katika mipaka yenu
ili kuwabaini magaidi na kukagua hati za kusafiria, wakati tulionao si wa kumuamini
kila mtu kwani leo anaweza kuwa mtu mwema na kesho akawa adui," alisema.
Kwa upande wake, Askofu Masangwa alisema kutokana na matukio hayo nchini Kenya,
Serikali ya Tanzania imeanza kuchukua tahadhari na kanisa limeanza kuimarisha
ulinzi kwenye nyumba za ibada zilizopo mipakani katika ibada.
Alitoa pole kwa Serikali ya Kenya kutokana na tukio la ugaidi lililowakuta hivi
karibuni na kusababisha watu 148 kupoteza maisha katika Chuo Kikuu cha Garissa.
Mkuu wa Jimbo la Arusha Magharibi, Mchungaji Isaac Kissiri, alisema tukio hilo
ni la kinyama na linapaswa kulaaniwa na watu wote wapenda amani.
Ili kuonesha ushirikiano uliopo kwa kanisa hilo upande wa Kenya na Tanzania,
Maaskofu hao, wachungaji, waumini na
wanakwaya walipanda miti 50 iliyotolewa na Halmashauri ya Longido katika eneo
la Kanisa ili kutunza mazingira
Chanzao Gazeti la Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment