Arusha
Home » » WIZARA YASABABISHA TANAPA KUPOTEZA MAPATO BILIONI 80/-

WIZARA YASABABISHA TANAPA KUPOTEZA MAPATO BILIONI 80/-

 
Mwenyekiti wa Kamati Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli.
 
Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), limepoteza zaidi ya Sh. bilioni 80, kwa kipindi cha mwaka 2011 hadi 2014, kutokana na Wizara ya Maliasili na Utalii kutotangaza sheria ya tozo ya wageni katika hoteli za kitalii kwenye Hifadhi za Taifa kwenye Gazeti la Serikali (GN).
Mwenyekiti wa Kamati Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, alisema mwaka 2011 Bunge lilipitisha Sheria ya ongezeko la tozo kwa wageni wanaofikia kwenye hoteli za kitalii hifadhini na Wizara kutakiwa kutangaza kwenye GN ili ianze kutumika.

Alisema baada ya Bunge kupitisha wafanyabiashara wa utalii mkoa wa Arusha walifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, na Tanapa ilishinda katika hukumu iliyotolewa Septemba 14, mwaka jana na siku kumi baadaye waliiandikia Wizara juu ya amri ya Mahakama ya kutaka tangazo kuwekwa kwenye GN.

“Miezi minne sasa serikali haijatangaza, kila mwaka Tanapa ingepata mapato ya Sh. bilioni 20 sawa na Sh. bilioni 1.5 kila mwezi, lakini kwa uzembe na matakwa ya wachache haijatangazwa fedha zinapotea kwa wenye mahoteli kutengeneza faida kubwa zaidi,” alisema na kuongeza:

“Kamati inajiuliza kigugumizi cha nini kwenye hili? walioshtaki wangekuwa na kigugumizi Mahakama ingesema, tunaishangaa serikali inapotaka kufanya jambo lake inawafikiria wadau zaidi huku wadau ahwaifikirii serikali.”

Lembeli alisema kabla ya Bunge kupitisha sheria hiyo tozo la kila mgeni lilikuwa ni Dola za Marekani tano hadi nane kwa anayelala kwenye vyumba vya Dola 100 hadi 150, na hadi sasa inapata kiasi hicho huku bei ya chumba kimoja ikiwa ni Dola 600,000.

Alisema inashangaza watendaji wa serikali hawako tayari kulinda maslahi ya serikli bali ya wafanyabiashara.

Naibu Waziri, Mahamood Mgimwa, alisema hadi Januari 28, mwaka huu, watakuwa wameweka tangazo hilo na litawasilishwa mbele ya Kamati.

Hata hivyo, NIPASHE ilimtafuta Waziri Lazaro Nyalandu (pichani), ambaye ametajwa kwenye ripoti iliyowasilishwa kwenye Kamati kuwa amekuwa chanzo cha ucheleweshaji huo, simu yake haikupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi haukujibiwa.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa