Arusha
Home » » MSHITAKIWA ADAI KUTESWA, KUDHALILISHWA POLISI

MSHITAKIWA ADAI KUTESWA, KUDHALILISHWA POLISI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MSHITAKIWA katika kesi ya ugaidi, Abdallah Maginga, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kumruhusu kutohudhuria siku za kesi na abaki magereza, kutokana na maumivu makali anayodai anayapata sehemu za siri alikominywa na polisi na kuingiziwa mti kwenye haja kubwa.
“Mheshimiwa Hakimu naomba mahakama yako inipe ruhusa ya kutohudhuria siku ya kesi, sababu ninapopanda gari napata maumivu makali sana sehemu za siri kunauma kwa sababu polisi walinitesa kwa kuniingizia mti kwenye haja kubwa na kuminya sehemu zangu za siri,” alisema.
Alisema mbele ya Wakili wa Serikali, Rose Sulle kuwa mbali na maumivu ya sehemu za siri, pia mguu wake uliokatwa hospitalini, bado unamsumbua kutokana na maumivu.
Maginga pia aliomba iagize Magereza wamruhusu akatibiwe hospitalini, kwani alitakiwa kwenda kupata matibabu Septemba 5 mwaka huu, ila alizuiwa hadi sasa.
Akijibu hoja hizo, Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo, Devotha Msofe, alisema suala la kuja mahakamani ni lazima na mahakama haiwezi kumpa ruhusa hiyo.
Pia, alimshauri mshitakiwa huyo kuwa kama ana maelezo mengi, amweleze hakimu anayesikiliza kesi yake, Mustapher Siyani ambaye kwa siku hiyo hakuwepo.
“Sikiliza Maginga suala la kuja mahakamani ni lazima na sio hiyari wala majadiliano, ila kuhusu kwenda hospitalini liwasilishe Magereza ndio mtaona kwa pamoja mnafanyaje,” alisema.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washitakiwa hao wameshitakiwa kwa makosa yaliyo chini ya Sheria ya Kuzuia ugaidi, ambapo Sheria Namba 22 ya Mwaka 2002 inasema upelelezi ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza na kutoa uamuzi.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na Al-Shabaab.
Mbali na mashitaka hayo, pia wanahusishwa na tukio la mlipuko wa bomu lilitokea baa ya Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.
Watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na mashitaka hayo ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabiti, Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajab Hemedi, Hassan Saidi, Ally Hamisi, Yassin Sanga, Shaaban Wawa, Swaleh Hamisi, Abdallah Yassin, Abdallah Maginga na Sudi Nassib Lusuma.
Wengine walioongezwa katika shauri hilo ni Shaaban Mussa, Athuman Hussein, Mohammed Nuru, Jafari Lema, Abdul Mohammed na Said Michael Temba.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa