Arusha
Home » » MAJAJI WAPONGEZWA KWA KUMALIZA VIZURI KESI ZA UCHAGUZI

MAJAJI WAPONGEZWA KWA KUMALIZA VIZURI KESI ZA UCHAGUZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na Lydia Churi-Mahakama
Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wengine wamepongezwa kwa kumaliza vizuri kesi za uchaguzi zilizofunguliwa katika Mahakama Kuu kanda mbalimbali nchini na pia kutenga muda wa kujadili changamoto zilizotokana na kesi hizo.

Akizungumza na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo jijini Arusha, Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman amewapongeza Majaji hao kwa kujitoa katika kusikiliza kesi hizo na kuzitolea hukumu kesi nyingi kwa kipindi kifupi licha ya kesi chache kubakia mahakamani.

Jumla ya kesi 53 za Ubunge zilizotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zilifunguliwa katika Mahakama Kuu kanda za Dar es salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya, Moshi, Mtwara na Mwanza. Kanda nyingine ni Shinyanga, Songea, Sumbawanga, na Tanga. Kati ya kesi hizo, kesi 31 zilimalizika katika hatua za awali na kesi 22 ziliendelea,  mpaka sasa kesi 19 zimemalizika. kesi tatu bado ziko mahakamani. 

Hata hivyo kesi zote 196 zilizotokana na uchaguzi wa madiwani zilimalizika mapema katika Mahakama  mbalimbali za Hakimu Mkazi nchini. Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kufanyika kwa uchaguzi Mkuu nchini, zaidi ya asilimia 94 ya kesi za uchaguzi zilizofunguliwa kwenye Mahakama Kuu zimemalizika wakati asilimia 100 ya kesi zote za udiwani zimemalizika.

Aidha, Jaji Mkuu amewataka Majaji hao kuweka mikakati ya kuhakikisha kasi ya kupunguza kesi mahakamani hasa zile za muda mrefu inaongezeka ili kupunguza malalamiko yanayotokana na kuchelewa kutoa hukumu na kutopatikana kwa nakala za hukumu kwa wakati. 

Mheshimiwa Chande amewataka Majaji kusimamia suala la maadili ndani ya Taasisi hiyo ili kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama yao. 

Kuhusu suala la Maadili kwa Mahakimu, Jaji Mkuu amesema wameomba ushauri Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa endapo hakimu atashtakiwa kwa kosa la rushwa ataondolewa kazini kwa maslahi ya Umma hata kama atashinda kesi hiyo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa