Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KESI ya wizi ya Sh bilioni saba inayowakabili waliokuwa wafanyakazi
14 wa benki ya Exim ya jijini Arusha, iliendelea kusikilizwa juzi na
jana. Shahidi wa pili katika kesi hiyo, Raymond Matiko (35) aliieleza
Mahakama kuwa miamala ya fedha za kigeni (dola), ilichukuliwa kutoka
katika akaunti sita zilizofunguliwa katika benki hiyo.
Matiko ambaye wakati huo wa wizi alikuwa Meneja wa Operesheni makao
makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam na pia Mkuu wa Kitengo cha
Mfumo wa Kielektroniki katika benki hiyo, alisema kuwa mfumo wa kisasa
wa elektroniki, ulianza katika benki hiyo mwaka 2010.
Shahidi huyo alikuwa akitoa ushahidi wake, akiongozwa na Mwanasheria
wa Serikali, Paul Kaduchi. Alidai kuwa akaunti hizo sita, zilifunguliwa
na wateja na zilitumika kukwapua miamala ya dola kutoka katika kampuni
mbalimbali za kitalii na watu binafsi waliokuwa wakiweka pesa katika
benki hiyo.
Alitaja akaunti na majina ya akaunti kuwa ni akaunti namba 5701555011
ya Nuru Benedicti Sanga, 0031023792 ya Mosses Chacha Aloyce, 0031023771
ya Gervas Fulgence Kimaro, 5795276654 ya Furahini Elibariki Ngoda,
5795340108 ya Tumaini Raphael Mwandingo na 0031023088 ya Raymond Allais
Telekish.
Alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Arusha/Arumeru, John
Kamugisha kuwa fedha hizo ziliingizwa na kuidhinishwa na baadhi ya
watuhumiwa katika akaunti hizo. Shahidi huyo alitoa kielelezo P2 ambacho
ni akaunti ya dola, iliyokuwa ikionesha jinsi maelfu ya dola
yalivyokuwa yakiingizwa, kuidhinishwa na kuhamishwa kutoka akaunti za
kampuni mbalimbali za kitalii na binafsi jijini Arusha na watuhumiwa
hao.
Hata hivyo, kielelezo hicho kilipingwa vikali kupokelewa na mawakili
wa watuhumiwa kwa kuwa hakikuidhinishwa na wakili, kama ni nyaraka
halali ya benki pamoja na kuwa na mhuri wa benki. Lakini, mwanasheria wa
serikali, Kadushi alijenga hoja ya kutaka Mahakama kukubali kielelezo
hicho kipokelewe mahakamani hapo na hakimu alikikubali.
Matiko alitaja baadhi ya kampuni za kitalii, zilizochotewa fedha zao
ni Kibo, Leopard, Ranger Safari na Bushback na kampuni nyingine za watu
binafsi. Shahidi huyo alidai walioidhinisha kuingiza maelfu ya dola
katika kaunti hizo maalumu ni watuhumiwa hao hao ; na walioidhinisha
kutoka ni watuhumiwa hao pia.
Katika kesi hiyo, wafanyakazi 14 na mfanyabiashara mmoja wanatuhumiwa
kuiba zaidi ya Sh bilioni saba kwa kughushi, utakatishaji fedha na wizi
wa mfumo wa kibenki kwa nyakati tofauti mwaka 2011 hadi 2012.
Wafanyakazi hao ni aliyekuwa Meneja wa Benki Tawi la Exim Arusha,
Bimel Gondalia (37), Lilian Mgaya (33), Neema Kinabo (30), Livingstone
Julius (36), Joyce Kimaro (36), Daud Mosha, Doroth Tigana (50) na Evans
Kashebo (40).
Wengine ni Mosses Chacha (37), Tuntufe Agrey (32), Joseph Meck (34),
Janes Massawe (32), Christophe Lyimo (34), Deodet Chacha (35) na Gervas
Gugo ambaye ni mfanyabiashara. Washitakiwa wanne ambao ni Gomes,
Kashebo, Neck na Lyimo, wapo nje kwa dhamana.
CHANZO: HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment