Arusha
Home » » WAOMBA MALIMBIKIZO YA WALIMU KULIPWA.

WAOMBA MALIMBIKIZO YA WALIMU KULIPWA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) wilayani Arumeru, kimeomba serikali kuharakisha malipo ya malimbikizo ya madeni yanayofikia Sh milioni 800 katika wilaya hiyo ili kuwawezesha walimu kufanyakazi kwa kasi zaidi.

Aidha, chama hicho jana kiliwaaga walimu wastaafu 31 wilayani humo na kuwapatia zawadi ya mabati 620, kila mmoja akipata mabati 20 kama kumbukumbu ya utumishi wa ualimu nchini.
Akizungumza jana wakati wa hafla ya kuwaaga waalimu hao, Katibu wa CWT wilayani Arumeru, Joyce Kijazi, alisema serikali ikiharakisha kulipa madeni ya walimu, itahamasisha utendaji kazi ulio bora zaidi.

Aliiomba serikali kuharakisha ulipaji wa madeni hayo yaliofikia Sh milioni 800 kwa wilaya hiyo, fedha ambazo ni mapunjo ya mishahara, mishahara ya nyuma, fedha za uhamisho, matibabu, mazishi na masomo.

Kijazi alisema madeni hayo ni malimbikizo ya tangu mwaka 2009. Kuhusu walimu waliostaafu, alisema zawadi hiyo ya mabati 20 kwa kila mmoja ni moja ya utekelezaji wa agizo lililotolewa katika mkutano mkuu wa CWT Taifa, uliokaa mwaka 2014 na kuazimia kuwapatia mabati 20 kwa kila mwalimu atakayestaafu kuanzia kipindi cha Julai 2015.
Walimu hao 31 walistaafu kati ya Julai na Septemba mwaka jana.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa