Arusha
Home » » VYAMA VYAMTAKA SIMBACHAWENE.

VYAMA VYAMTAKA SIMBACHAWENE.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene 
 Vyama vinne vya wafanyakazi mkoani hapa vimemuomba Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, kufanya ziara na kuzungumza na viongozi wake ili kuzipatia ufumbuzi kero za muda mrefu na kuleta tija kazini.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe) mkoani hapa, Samwel Magero akisoma tamko kwa niaba ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (Talgwu) na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (Raawu), alisema wametoa ombi hilo baada ya ngazi za chini kushindwa.
Juzi, kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Halmashauri ya Arusha kilivunjika baada ya viongozi wa vyama hivyo kudai kupata wito wa kuhudhuria kutoka kwa mwenyekiti ambaye ni mkurugenzi mtendaji wakati ujumbe wao katika baraza hilo ulikoma mwaka 2011.
Alisema licha ya kasoro hiyo, pia waligomea kikao cha bajeti ya halmashauri baada ya kubaini makabrasha waliyopewa yalikuwa na kurasa 35 badala ya kurasa 106.
“Tumegomea kikao hicho kutokana na wajumbe kukosa sifa. Pia mchanganuo wa bajeti za idara muhimu hazimo ambazo ni afya, maji na elimu na halmashauri zote katika Mkoa wa Arusha zimo, isipokuwa ya Monduli haina mabaraza halali ya wafanyakazi. Pia, kuna madai ya fedha za watumishi zaidi ya Sh120 milioni hazijalipwa tangu 2012,” alisema.
Katibu wa CWT wa mkoa huo, Hassan Said alisema baraza hilo lilipaswa kufanya vikao viwili kwa mwaka, lakini wenyeviti wamekuwa wakiitisha kimoja cha bajeti ambacho hakitoi nafasi ya majadiliano na mwajiri ili kupunguza changamoto.
“Tunamuomba waziri aje kuzungumza na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kujadiliana matatizo kati ya wanafanyakazi na viongozi wa wilaya, mkoa na sisi,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha, Fidelis Lumato alisema kesho watakuwa wamepata wajumbe halali ili kujadili bajeti .

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa