Arusha
Home » » JAJI SAMATA, PROF. SAFARI WATOA USHAHIDI KESI YA DK. SLAA

JAJI SAMATA, PROF. SAFARI WATOA USHAHIDI KESI YA DK. SLAA

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa.
Shahidi wa kwanza wa kesi ya jaribio la kumtapeli Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa, Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Hai, kwamba hakuwahi kumpigia simu kiongozi huyo akimtaka  ampe
fedha ili akisaidie chama chake kushinda kesi ya rufaa katika Mahakama Kuu ya Arusha.

Kesi hiyo  iliyofunguliwa kupinga hukumu ya kumvua ubunge Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Rufaa hiyo namba 47 ya mwaka 2012 ilifunguliwa na Lema dhidi ya Mussa Hamis na wenzake, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu ya Arusha ya  kuvuliwa ubunge ambapo hata hivyo, ilikwishatolewa uamuzi na Lema kurejeshewa ubunge wake.

Samatta akiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Denis Mpelembwa aliiambia mahakama kwamba hakuwahi kumpigia simu Dk. Slaa kwa sababu tangu astaafu nafasi yake ya Jaji Mkuu mwaka 2007, hajawahi kufika mkoani Kilimanjaro kama inavyodaiwa kuwa alimpigia simu akiwa katika baa ya Florida, mjini Moshi.

Jaji Samatta aliiambia mahakama kuwa Aprili 6, 2012, Dk. Slaa alimtumia ujumbe, akitaka kujua kama ujumbe aliomtumia kupitia simu ya mkononi (0754013237) iliyosajiliwa kama Abeid  Adam Abeid ni wa kwake na yeye akamjibu kwamba siyo ya kwake wala hamfahamu mtu aliyetuma ujumbe huo.

“Ni kweli mimi kama raia wa kawaida niliifahamu kesi ile kupitia vyombo vya habari kwamba Godbless Lema (Mbunge wa Arusha Mjini) kupitia Chadema alikuwa amekata rufaa kupinga hukumu ya kuvuliwa ubunge wake, lakini baadaye nilimtaka suala hilo lisiishie kisiasa bali liamuliwe kisheria,” Jaji Samatta aliieleza mahakama.

Kesi hiyo namba 47 ya mwaka 2012 iliyofunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Hai, ikimkabili mshitakiwa Abeid Abeid, inao mashahidi 12, akiwamo Jaji Samatta, Profesa Abdallah Safari, Dk. Slaa na Lema.

Hata hivyo, shahidi wa pili katika shauri hilo, Profesa Safari ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, akiwa alidai kuwa  alipigiwa simu na mtu aliyejiita kuwa ni Jaji Samata, akimuomba ampatie namba za Lema, lakini kabla ya kufanya hivyo, aliwasiliana kwanza na Lema ambaye hata hivyo alimjibu kwamba mtu huyo hapatikani kwenye simu yake.

”Nikiwa njiani kuelekea Bunju-Tegeta, nilipigiwa simu na mtu nisiyemfahamu, namba zake nazikumbuka ni 0754013237, aliponipigia aliniambia anataka namba za Lema, nilimpa baadaye, lakini kwa kuwa sauti yake pia  niliitilia shaka, nililazimika kuwasiliana na mtendaji mkuu wa chama ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema Taifa (Dk. Slaa) ili afuatilie", alidai Profesa Safari.

Aliongeza kuwa  muda mfupi baada ya kufika shambani kwake huko Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Lema alimpigia na kumwambia kwamba
mhusika wa namba hiyo (0754013237) hapatikani tena.
 

CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa