Arusha
Home » » TBL YATUMIA MIL. 80/- WIKI YA NENDA KWA USALAMA BARABARANI

TBL YATUMIA MIL. 80/- WIKI YA NENDA KWA USALAMA BARABARANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
TBL yatumia mil. 80/- wiki ya nenda kwa usalama barabarani
 KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), imetumia sh milioni 80 kufanikisha shughuli mbalimbali wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama barabarani nchini.

Hayo yalisemwa na Ofisa Uhusiano wa TBL, Dorris Malulu, wakati wa zoezi la upimaji afya kwa madereva wa mabasi na magari ya mizigo lililofanyika kituo cha kupimia uzito magari Makuyuni wilayani Monduli mkoani Arusha.
Malulu, alisema wameamua kufadhili madhimisho hayo kutokana na ukweli kwamba, TBL ni wadau wakubwa wa usalama barabarani, ukizingatia kwamba bidhaa zao zinasafirishwa kwa njia ya barabara hadi kuwafikia wateja wao.
Katika fedha hizo, alisema zimetumika katika upimaji wa afya, kugawa vipeperushi, stika, fulana, kofia na shughuli nyinginezo huku akibainisha mwaka huu walilenga kuwafikia madereva 2,000 katika vituo vya Mikese, Msata na Makuyuni.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu, Dk. Charles Msenga, alisema katika kituo cha Mikese walifanikiwa kuwapima afya madereva 800, wakati Msata walikuwa 600 na Makuyuni 800.
Akizungumzia hali waliyoikuta wakati wa zoezi hilo, Dk. Msenga, alisema wamewakuta baadhi ya madereva wakiendesha magari huku Shinikizo la Moyo (BP), likiwa juu kwa kiwango cha 217 kwa 125 na dereva huyo alikuwa amebeba abiria 60, hivyo kulazimika kumpumzisha kwa muda na kumpatia dawa.
“Pia madereva wengi tumekuta macho yao yana uono hafifu ama kwa macho yote au jicho moja, ambapo hawa  tumewapa ushauri na kuwataka waendelee na matibabu ama kwa kupewa miwani itakayowasaidia kuona vizuri,” alisema Dk. Msenga.
Naye Mratibu wa Huduma za Macho Jiji la Arusha, Dk. Juraj Msuya, alisema dereva wa gari anatakiwa kila baada ya miezi mitatu awe anapima macho yake ili kujua yana kiwango gani cha kuona wakati akiwa anaendesha chombo cha usafiri.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Jowika Kasunga, aliyekuwa mgeni rasmi katika zoezi hilo, aliwashukuru TBL kwa kufanikisha upimaji wa afya za madereva kwa madai kuwa, zoezi hilo lina gharimu kiasi kikubwa cha fedha.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Mohamed Mpinga, alitoa wito kwa madereva kote nchini kujenga tabia ya kupima afya zao pindi wanapopata nafasi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa