Arusha
Home » » KINARA WA UGAIDI AUAWA ARUSHA

KINARA WA UGAIDI AUAWA ARUSHA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

JESHI la polisi Mkoa wa Arusha limemuua kwa kumpiga risasi mtuhumiwa wa ugaidi, Yahaya Hassan Omari Hela (31) ‘Yahaya Sensei’ mkazi wa Mianzini mjini hapa.
Mtuhumiwa huyo alipigwa risasi ya mguu na kalio la kulia eneo ya Kisongo wilayani Monduli alijaribu kuruka kwenye gari la polisi kwa lengo la kuwatoroka.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 19 mwaka huu saa 5 usiku wakielekea kijiji cha Chemchem wilayani Kondoa, Dodoma alikozaliwa mtuhumiwa huyo ili akawaoneshe alipohifadhi mabomu.
Alisema mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa mwalimu wa Karate na Judo alikuwa muasisi na kinara wa matukio ya ugaidi yaliojitokeza Jijini Arusha, Zanzibar, Mwanza na Dar es Salaam.
Kamanda Sabas, alisema walifanikiwa kumkamata baada ya kumtafuta muda mrefu kwa kutumia intelijensia ya polisi ya kisasa na hali ya juu kabla ya kumkamata mkoani Morogoro Oktoba 6 na kupelekwa Arusha Oktoba 11.
Alisema mtuhumiwa huyo alipohojiwa alikiri kuratibu matukio mbalimbali ya ugaidi.
Baada ya kupigwa risasi hizo alifariki dunia akiwa njiani kuwahishwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa matibabu na kwamba mwili wake katika hospitali hiyo.
Sabas aliyataja baadhi ya matukio mtuhumiwa huyo aliyokiri kuhusika kuwa ni lile la Oktoba 25, 2012 saa 5:30 usiku katika mtaa wa Kanisani Paloti kata ya Sokoini One jijini hapa ambapo yeye na wenzake walitega bomu nyumbani kwa Abdulkarim Idd Jonjo (52) katika chumba alicholala na kumjeruhi.
Kamanda Sabas alisema mtuhumiwa huyo alikiri kushiriki tukio la Mei 5 mwaka 2013 saa 10:30 eneo la Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililopo Olasiti jijini Arusha ambapo aliratibu kurushwa kwa bomu na kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi 56.
Tukio la tatu lilitokea Juni 15 mwaka 2013 saa 11:50 jioni katika Viwanja vya Soweto Kata ya Kaloleni Jijini Arusha, ambapo marehemu na wenzake walirusha bomu na kujeruhi watu 60 na wanne kufariki dunia waliokuwa kwenye mkutano wa kufunga kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kamanda Sabas Alitaja matukio mengine aliyokiri kuhusika nayo ni lile la Julai 11 mwaka 2013 eneo la kwa Mrombo jijini hapa, ambapo alishirikiana na wenzake kumwagia tindikali usoni Sheikh Said Juma Makamba.
Tukio jingine ni lile la Februari 12 mwaka 2014 saa eneo la Tindigani Unga limited jijini hapa kwenye msikiti wa Sawiyatu Qadiria, walipommwagia tindikali usoni Sheikh Hassan Bashir.
Tukio la sita la Februari 28 mwaka 2014 saa 5:15 alfajiri huko msikiti wa Bondeni Jijini Arusha, marehemu na wenzake walimwagia tindikali Mistapha Mohamed Kiago na kumjeruhi usoni na shingoni.
Tukio la saba Aprili 13 mwaka 2014 saa 1:30 usiku, eneo la Mianzini, huko nyumba ya kulala wageni na Baa ya Night Park, walirusha bomu na kujeruhi watu kumi na mtu mmoja kusababisha kifo chake.
Kamanda alitaja tukio lingine aliloshiriki ni la Aprili 13 mwaka 2014 la saa 5 eneo la Majengo jijini Arusha, alirusha bomu kwa kushirikina na wenzake na kujeruhi watu wawili Sudi Ali Sudi (37) ambaye ni Mkurugenzi wa Answar Muslim kanda ya Kaskazini na mwenzake Muhaji Hussein Kifea (38) mkazi wa Dare s Salaam.
Tukio la tisa mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa Julai 7 mwaka 2014 saa 4:15 usiku eneo la uzunguni, mgahawa wa vama Traditional Indian uliopo jirani na Viwanja vya Gymkhana alirusha bomu na kujeruhi watu nane.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa