Arusha
Home » » SAMSUNG YATOA ELIMU KUGUNDUA BIDHAA FEKI

SAMSUNG YATOA ELIMU KUGUNDUA BIDHAA FEKI

KUTOKANA na kuongezeka kwa wimbi la bidhaa feki zinazoingizwa nchini, Kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Samsung imewataka wananchi wanaonunua bidhaa zake kuzisajili kwenye namba maalum itakayowawezesha kubaini kama bidhaa hiyo ni halisi.
Aidha, kwa kufanya hivyo itawawezesha kupata usajili wa bidhaa hiyo, hivyo kupatiwa huduma ya matengenezo bure endapo kitapata hitilafu ndani ya miaka miwili tangu kinunuliwe.
Hayo yalibainishwa juzi na Mkurugenzi wa kampuni hiyo hapa nchini, Mike Seo, wakati alipokuwa akifungua kituo cha huduma kwa wateja jijini hapa kitakachotumika kuuza bidhaa hizo pamoja na kufanyia matengenezo.
Alisema kuwa kwa kutumia mfumo huo wa kusajili vifaa, utawawezesha wananchi kuepuka kununua bidhaa bandia, kwani atapata majibu moja kwa moja wakati akisajili bidhaa kwenye huduma ya ‘e warranty’ (dhamana).
“Hivi karibuni kumekuwa na utitiri wa bidhaa bandia na zilizo kinyume cha sheria kuingizwa nchini kiholela. Ukiwa mteja wa bidhaa za Samsung utafaidika na bidhaa zetu, kwani tunatoa ‘warranty’ (dhamana), ya miezi 24,” alisema Seo.
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma wa kampuni hiyo, Mubaraka Mikidadi, alisema duka hilo litawaondolea usumbufu wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, ambao awali walitegemea kituo cha Dar es Salaam kwa ajili ya matengenezo ya bidhaa zao pindi zinapopata hitilafu.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa