Arusha
Home » » NI BANGI TENA

NI BANGI TENA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limefanikiwa kuwakamata watu wawili wakiwa wanasafirisha magunia manne ya  madawa ya kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilogramu 173.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas amesema kwamba, watu hao walikamatwa juzi saa 5:00 usiku katika eneo la Nduruma jijini hapa ambapo walikuwa wanasafirisha madawa hayo kwa kutumia gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T. 592 AAP.

Aliongeza kwa kusema kwamba, mafanikio hayo yalipatikana kutokana na ushirikiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi Mkoani hapa na wananchi ambao walitoa taarifa juu ya tukio hilo. Alisema mara baada ya taarifa hiyo askari wa kitengo cha kuzuia Madawa ya Kulevya mkoani ambao waliokuwa doria usiku huo waliweka mtego eneo la Nduruma na kufanikiwa kulisimamisha gari hilo lililokuwa linatokea eneo la Olkokola wilayani Arumeru kuelekea Tanga.

‘’Mara baada ya upekuzi walifanikiwa kuyaona magunia hayo ambayo yaliwekwa katika sehemu mbili; gunia moja lilikuwa kwenye ‘’boot’’ na magunia matatu yalikuwa kwenye ‘’Seat’’ ya katikati. Alisema Kamanda Sabas.

Akiwataja watuhumiwa hao Kamanda Sabas alisema kuwa ni Laizer Melau (35) Mkazi wa Olkokola wilayani Arumeru na Richard Fanuel (38) Mkazi wa Mianzini Jijini hapa pia ni dereva wa gari hilo. Alisema mara baada ya mahojiano watuhumiwa hao wamekiri kuhusika na tukio hilo na watafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika.

Kamanda Sabas aliendelea kuwashukuru wananchi wa Arusha kutokana na ushirikiano wao mkubwa katika utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu na kuwaomba waendelee kufanya hivyo na Jeshi hilo litaendelea kuzifanyia kazi hali ambayo itasaidia kudumisha hali ya amani na utulivu.
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa