Arusha
Home » » CHADEMA WAIBWAGA SERIKALI, WABUNGE WAKALIA KUTI KAVU

CHADEMA WAIBWAGA SERIKALI, WABUNGE WAKALIA KUTI KAVU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
komuALIYEKUWA Mgombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, (EALA), kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Anthony Komu, ameibwaga Serikali kwenye kesi aliyoifungua Mahakama ya Afrika Mashariki, (EACJ), baada ya maombi yake mawili kukubaliwa huku moja likitupwa.
Mahakama hiyo, imesema kuwa kuwa  Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilikiuka kipengele cha 50 (1) cha uanzishwa wa jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye uchaguzi uliofanyika Aprili 17, 2012.
Uamuzi huo wa shauri hilo namba 7/ 2012 la kutaka tafsiri ya kipengele hicho, ulitolewa jana na Jaji Mkuu wa mahakama hiyo, Jean Bosco Butasi kwa saa 1:20 kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 4:20 asubuhi kwenye mahakama hiyo iliyopo jengo la makao makuu ya EAC, Arusha.
Alisema kuwa kitendo cha Bunge la Tanzania kutengeneza  makundi manne ya wagombea kwa kigezo cha jinsia, Zanzibar, vyama vya upinzani na Tanzania Bara, ambayo wagombea wote walitokana na vyama vya siasa, ulikinzana na kanuni ya 50 (1) ya mkataba wa uanzishwaji wa EAC inayotaka kuwe na ushiriki wa makundi mbalimbali ya jamii.
Jaji huyo, alisema kuwa, pia kuruhusu mgombea kutoka chama cha siasa cha Tadea, Lifa Chipaka kushiriki uchaguzi huo kutoka kundi la vyama vya siasa wakati chama hicho kikiwa hakina uwakilishi bungeni ni kinyume na kipengele hicho cha mkataba, huku akishauri kuwa angeweza kugombea kupitia makundi mengine ndani ya jamii.
Aidha, mahakama hiyo ililionya bunge hilo kuhakikisha katika chaguzi zake zinazofuata kuwa makini kuhakikisha mkanganyiko wa aina hiyo haujirudii.
“Suala la kama wabunge wanaoiwakilisha Tanzania kwenye EALA wamechaguliwa kihalali au hapana, litaamuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania,” alisema Jaji huyo wakati akisoma uamuzi huo.
Aidha, aliuagiza upande wa wajibu maombi, Mwansheria Mkuu wa Serikali, kumlipa mleta maombi, Komu robo ya gharama alizotumia kwenye shauri hilo.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupa ombi moja lililowasilishwa mahakamani hapo na Komu, akitaka kwa kuwa CHADEMA ni chama kikuu cha upinzani, kilipaswa kupata nafasi kwenye bunge la EALA badala ya nafasi hiyo kupewa vyama vyenye idadi ndogo ya uwakilishi wa wabunge.
Kwa upande wao mawakili wa Komu, Edson Mbogoro na John Mallya, walisema wamerikidhika kwa uamuzi huo huku wakisema kuwa, sasa wanajielekeza kwenye shauri walilolifungua Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.
Mallya, alisema kuwa kwenye shauri hilo namba 1/2012 litakalorudi mahakamani hapo kwa ajili ya kupanga tarehe za kuendelea na usikilizwaji Novemba 27 mwaka huu, wanaiomba mahakama hiyo itengue matokeo ya uchaguzi wa wabunge wa EALA, kutokana na ukiukaji wa kanuni ikiwemo kipengele cha 50 (1) cha mkataba wa uanzishwaji wa EAC.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Nkasari Sarakikya, aliyekuwa akishirikiana na Pius Mboya na Mark Mukwamo, alisema kuwa wanasubiri kupata nakala ya uamuzi huo waupitie ndipo waweze kujua nini cha kufanya.
 Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa