Arusha
Home » » WATUHUMIWA KESI YA UGAIDI WAHOJI ALIPO MWENZAO

WATUHUMIWA KESI YA UGAIDI WAHOJI ALIPO MWENZAO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Watuhumiwa wa kesi ya ugaidi na kudaiwa kufanya uwakala wa kusajili vijana kujiunga kundi la Al- Shabaab la nchini Somalia wameutaka upande wa Mashitaka kuwaeleza alipo mtuhumiwa namba mbili, Abdallah Thabit.
Malalamiko hayo yaliyotolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa ya Arusha, Rose Ngoka, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa. 

Mtuhumiwa mmoja katika kesi hiyo alinyoosha mkono na kumuomba Hakimu Ngoka auulize upande wa Mashitaka ni kwanini hadi jana wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa Thabit hakuwa amefikishwa mahakamani.

“Mheshimiwa Hakimu Julai 24, mwaka huu upande wa Mashitaka ulidai kwamba ungemleta mtuhumiwa Thabit, lakini mpaka leo (jana) hatujui ni kwanini hajaletwa mahakamani,” alisema mtuhumiwa, Ally Hamis.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Gaudencia Joseph, alidai kwamba ndiyo mara yake ya kwanza kusimamia taarifa hiyo, hivyo atakwenda kuifanyia kazi.

“Mheshimiwa Hakimu, taarifa hii ndiyo naisikia leo (jan) hapa, na hii ni kwa sababu Mwendesha Mashitaka anayesimamia shauri hili hayupo, hivyo sikuwa na taarifa kama walishawahi kuwasilisha malalamiko yao.

“Lakini tarehe ijayo naamini watapata taarifa za mshitakiwa mwenzao kwanini hajaletwa kama walivyodai mbele yako. Lakini pia upelelezi wa shauri hili haujakamilika, hivyo tunaomba tena tarejhe nyingine ya kutajwa,” alisema Joseph. Majibu  hayo yalionekana kutomridhisha mtuhumiwa huyo na kumuomba tena Hakimu Ngoka nafasi na kusisitiza kuwa hata Julai 24, mwaka huu majibu yaliyotolewa ni kama hayo.

Hata hivyo, Hakimu Ngoka aliingilia kati na kutoa ufafanuzi kwamba majibu sahihi yangeweza kutolewa na Mwendesha Mashitaka aliyekuwapo  kwani hata hakimu anayesikiliza shauri hilo naye hakuwapo.

“Tatizo ni kwamba hakimu na mwendesha mashitaka wote hawapo leo (jana), tunaiahirisha kesi hii hadi Septemba 3, mwaka huu,” alisema Hakimu Ngoka.

Washitakiwa  hao wameshitakiwa kwa makosa yaliyo chini ya Sheria ya kuzuia ugaidi, namba 22  ya mwaka 2002 inayosema upelelezi ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza na kutoa uamuzi

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na Al-Shabaab.
Pia, wanahusishwa na  tukio la  mlipuko wa bomu katika baa ya Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.

Washitakiwa hao ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabit, Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajabu Hemed, Hassan Said, Ally Hamisi, Yasini Sanga, Shaabani Wawa, Swalehe Hamisi, Abdallah Yasini, Abdallah Maginga na Sudi Nasibu Lusuma.

Wengine walioongezwa katika kesi hiyo ni Shaban Musa, Athuman Hussein, Mohamed Nuru, Jafari Lema, Abdul Mohamed na Said Michael Temba.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa