Arusha
Home » » WANAWAKE ARUSHA WAZIDI KUISHI KWA HOFU

WANAWAKE ARUSHA WAZIDI KUISHI KWA HOFU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
WANAWAKE jijini Arusha, wamesema usalama wao uko matatani kutokana na kuongezeka kwa matukio yanayowalenga ya kushambuliwa kwa risasi na watu wanaokuwa kwenye bodaboda, ambako wengine wakijeruhiwa vibaya huku wawili wakifariki dunia.
Aidha, wameitaka Serikali kuangalia namna bora ya kukabiliana na wahalifu hao, kwani kwa sasa baadhi ya wanawake wameacha kuendesha magari na kuamua kutumia usafiri wa umma huku wengine wakiamua kutumia gari moja zaidi ya watatu.
Hayo yalisemwa jana na baadhi ya wanawake waliyojitokeza mbele ya jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, kuitikia wito wa ujumbe mfupi wa maneno uliyowataka kufika hapo, ingawa walitawanyika baada ya kukosa mtu wa kuwapa muongozo juu ya namna ya kukutana na kiongozi huyo.
Mmoja wa wanawake hao, Glory James, Mkazi wa Sanawari, alisema kuwa bado hawajaridhishwa na namna jeshi la polisi linavyoshughulikia suala la kupigwa risasi wanawake wanaoendesha magari jijini hapa, ambako wale waliyojeruhiwa hawakunyang’anywa kitu chochote huku wengine wakichukuliwa vito vya thamani, fedha na simu za kiganjani.
“Mimi na wenzangu baada ya kupokea ujumbe uliyotaka wanawake kufika kwenye ofisi za RC leo (jana), tuliamua kwanza kwenda kwa RPC ili kujua kama ni mkusanyiko halali.
“Alituambia si halali na akatushauri hakuna haja ya kwenda kwa RC, kwani tayari wameshakamata watu saba na akatuonyesha na silaha walizokamata, sisi bado hatujaridhika kwani bado matukio yanaendelea na hatujui sababu za matukio hayo na kwa nini walengwa ni wanawake tu,” alisema Glory.
Mwanamke mwingine mkazi wa Sakina, Neema Mollel, alisema yeye alifika mbele ya jengo la RC baada ya kupata ujumbe wa simu ya mkononi na kutokana na kuishi kwa wasiwasi, akaona akaungane na wenzake kupaza sauti ili Serikali iamke kuimarisha ulinzi kwa raia hasa wanawake.
Naye Lilian Cornelius, mkazi wa Ilboru, alisema ni vema wanawake na wananchi wa Arusha, wakatoa ushirikiano kwa kutoa taarifa polisi, kwani wahalifu hao wanaishi jijini hapa hivyo wanawafahamu, kwani kama si waume zao ni kaka zao au mahawara zao.
Kwa upande wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Sabas alisema aliwasihi wanawake hao kutofanya maandamano, kwani hatua dhidi ya matukio ya uhalifu zimechukuliwa na watuhumiwa saba hadi sasa wamekamatwa, hivyo akawataka watulie waliachie jeshi la polisi lifanye kazi yake
Chanzo;Tanzania Daima 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa